
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi, amekuwa mgeni rasmi katika mtoko wa Pasaka uliofanyika kwenye ukumbi wa kifahari wa Super Dome, Masaki – Dar es Salaam. Tukio hilo lilihudhuriwa na waumini, viongozi wa dini, na wageni mbalimbali waliokusanyika kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Pasaka kwa ibada na tafakari ya pamoja.

Akizungumza mbele ya umati ulioujaa ukumbi huo, Dkt. Nchimbi alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na maadili mema katika jamii, hasa katika kipindi hiki cha kiroho ambapo waumini wa Kikristo wanaadhimisha kufufuka kwa Yesu Kristo.

“Pasaka ni kipindi cha msamaha, upendo na kusameheana. Ni fursa ya kila mmoja wetu kutafakari maisha yake na kufanya maamuzi ya kuishi kwa kuzingatia haki, maadili na mshikamano wa kweli,” amesema Dkt. Nchimbi.
Aidha, alitoa rai kwa vijana kuendelea kuwa chachu ya maendeleo nchini huku akiwataka viongozi wa dini kushirikiana na serikali katika kujenga jamii yenye maadili, ustawi na uzalendo.
Mtoko huo ulipambwa na nyimbo za injili, maombi ya pamoja, na ujumbe wa matumaini kwa Taifa. Saa 24 itaendelea kukuletea matukio muhimu kama haya yanayoibua maadili na mshikamano katika jamii.