Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo hivi habari itakayofanyika April 29, mwaka huu Jijini Arusha.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo aprili 24,2025, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO Bw. Rodney Thadeus amesema maadhimisho hayo yatotatoa nafasi nzuri kwa wadau wa sekta ya habari, mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia kujadili masuala muhimu yanayohusu tasnia hiyo.
“Lengo kuu la maadhimisho hayo ni kulinda na kuboresha uhuru wa vyombo vya habari na kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi zao kwa uhuru na salama, hii pia itakuwa ni fursa ya kujadili usawa wa kijinsia na changamoto za kisera zinazohusiana na uendeshaji wa vyombo vya habari “.
Amesema siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani itatumika kama fursa ya kuweka mkazo mkubwa katika uhuru wa kujieleza ndani ya ajenda ya jumla ya haki za binaadam, siku hii pia itatumika kuanandaa hafla zinazoangazia uhusiano kati ya uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na haki zingine
Kwa upande wake Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) Susan Namondo amesema siku hiyo ni muhimu sana kwani Dunia kwani mchango wa vyombo vya habari ni mkubwa katika maendeleo ya nchi mbalimbali ambapo Tanzania imepiga hatua katika kusimamia uhuru huo.
Amesema kama ilivyo kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu, uhabarishaji kwenye dunia mpya, mchango wa akili mnemba kwenye uhuru wa vyombo vya habari, utasaidia tasnia hiyo kuzingatia mambo hayo
Maadhimisho hayo yameandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Habari-MAELEZO kwa kishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Umoja wa Mataifa (UN), Washirika wa Maendeleo, Waandishi wa Habari, Vyombo vya Habari za Mtandaoni na nje ya mtandao, Mashirika ya Kiraia, Watetezi wa Haki za Binaadam, watafiti, wasomi na Wadau mbalimbali wakiongozwa na taasisi ya Jamii Afrika.