Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekuwa miongoni mwa taasisi zilizoshiriki maonesho ya sekta ya ujenzi yaliyofanyika katika viwanja vya Mapinduzi Square Kisonge mjini Zanzibar.
Afisa Mkuu wa Mauzo na Masoko wa NHC, Bw. Daniel Kure, amesema kuwa ushiriki wa NHC katika maonesho hayo ni kuwafahamisha wakaazi wa Zanzibar kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na NHC, ikiwemo Morocco Square, 711 Kawe, Iyumbu, Samia Housing Scheme awamu ya pili, na ujio wa nyumba za makazi Kijichi.
Mkazi wa Zanzibar, Yahya Selemani, aliyefika banda la NHC, amesema kuwa uwepo wa NHC katika maonesho hayo utaleta hamasa kwa wakaazi kuchangamkia fursa ya kumiliki nyumba nje ya visiwa hivyo.
“Uwepo wenu hapa ni faida kubwa sana kwetu kwani tunapenda kumiliki nyumba mbali ya hapa lakini hatukuweza kupata fursa ya kufahamu vyema upatikanaji wa nyumba hizo. Sasa kazi kwetu miradi tumeifahamu, acha tuichangamkie,” amesema Selemani.
NHC inaendelea na nia yake ya dhati kuhakikisha wananchi wanamiliki nyumba kwa kuendelea kushiriki katika maonesho mbalimbali ili wananchi waweze kupata uelewa zaidi wa namna ya kumiliki nyumba kupitia miradi inayotekelezwa nchini.