Bajeti ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka wa fedha 2025/26 imesomwa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Dkt. Mohamed Mchengerwa, ambapo jumla ya kiasi cha shilingi trilioni 11.783 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za wizara hiyo na taasisi zake.
Hii ni ongezeko kutoka bajeti ya mwaka uliopita ambayo ilikuwa trilioni 10.125, hatua ambayo imeonekana kama ishara ya dhamira ya serikali kuimarisha huduma za kijamii nchini. Hata hivyo, licha ya kuongezeka kwa bajeti hiyo, baadhi ya wadau wameeleza wasiwasi wao kuhusu maeneo muhimu ambayo bado yanahitaji kupewa kipaumbele zaidi, hasa katika sekta ya elimu na afya.
Rebecca Mjema, mtaalamu wa masuala ya jinsia na uchumi, amesema bado kuna changamoto kubwa kwa watoto wa kike na wenye mahitaji maalum katika mazingira ya shule. Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa serikali kuhakikisha kuwa miundombinu inayojengwa inazingatia mahitaji ya watoto wa kike, hasa kipindi cha hedhi.
“Tulitegemea kuona miundombinu inayojengwa mashuleni ikiwa na vyumba maalum kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri wakati wa hedhi, pamoja na vifaa vya kuwasaidia kipindi hicho. Hadi sasa bado hakuna mazingira hayo katika miradi ya miundombinu inayopitia bajeti hii,” amesema Mjema.
Aidha, ameiomba serikali kuhakikisha kuwa kupitia bajeti ya mwaka 2025/26, kunakuwa na uboreshaji wa huduma za afya katika maeneo ya vijijini, ambako bado wananchi wanapata huduma kwa shida, hasa wanawake na watoto.
Kwa upande wake, Rhoda Mdoa, ambaye ni mmoja wa wadau waliotoa maoni yao, amesema serikali inapaswa kuhakikisha kuwa bajeti hii inatekelezwa kwa vitendo badala ya kubaki kwenye makaratasi. Amesema kuwa wananchi wanahitaji kuona huduma zikitolewa kwa haraka na kwa ufanisi.
Wadau hao wamesisitiza kuwa utekelezaji wa bajeti kwa ufanisi ndio kipimo halisi cha mafanikio ya mipango ya maendeleo, na kwamba ni muhimu kwa serikali kuendelea kusikiliza maoni ya wananchi ili bajeti hizi ziwe na manufaa kwa wote.