Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV- Dodoma
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira amesema Chama hicho kinawashukuru viongozi wa dini kwa ushauri wao wa kuhakikisha nchi naendelea kuwa na amani hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu na kubariki uchaguzi huo uendelee.
Pia amesema CCM haiwezi kupuuza ushauri unaotolewa na wadau mbalimbali katika kuelekea uchaguzi huo, lakini imesisitiza hautaahirishwa kwa kuwa mageuzi na mabadiliko ni jambo endelevu na haiwezi kuwa hoja ya kuahirisha uchaguzi.
Akizungumza leo Aprili 24,2025 wilayani Chamwino mkoani Dodoma alipokuwa akipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 ,Wasira amesema anawashukuru viongozi wa dini kwa ushauri na maoni yao kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu,
“Uchaguzi utaendelea sio kwamba tunapuuza mawazo, tutaendelea kuzungumza mambo ambayo yanaendelea, na tunashukuru sana nchi imetulia. Viongozi wetu wa kiroho wametuongoza wametupa ushauri mzuri sana na mimi nashukuru sana kwa kututia moyo na kutuambia uchaguzi uendelee lakini kwa amani,” amesema Wasira ambaye ameanza ziara ya siku tano katika mkoa huo.
Amesema kwamba CCM ni Chama kinachozungumza na kuhimiza amani ndio maana taifa limekuwa na utulivu kwa miaka 60, alisisitiza kwamba hilo linafanya Chama kijivunie kwa kuwa ni ushahidi kwamba kinaweza kusimamia amani.
Ameongeza haki iko ndani ya amani na kwamba ukiondoa amani utavunja haki za watu wengi hususan wanyonge, “ukiondoa amani watakaoumia hasa ni wanawake, watoto na walemavu.”
“Amani ni lazima sasa kuna wanaosema haki, na sisi tunasema ndani ya amani kuna haki, na haki hiyo inalindwa na amani kwa sababu ukiiondoa watu wengi wataathirika wala sio mtu mmoja ni wengi sana na ushahidi wake upo.”