
Maandalizi ya Tamasha kubwa la kiroho la “Twen’zetu kwa Yesu” yameanza rasmi kwa mwaka huu wa 2025, huku likitarajiwa kufanyika mara mbili tofauti kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake mwaka 2014.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Katibu Mkuu KKKT-DMP, CPA Goodluck Nkin, amesema kuwa , tamasha la kwanza litafanyika tarehe 19 Juni, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City likiwa ni maalum kwa watu wazima na wadau wa kada mbalimbali.
CPA Nkin amesema tamasha hilo limepewa jina la “Twen’zetu kwa Yesu Corporate Event” na linatarajiwa kuwahusisha watu 1,600 pekee. Viingilio vitakuwa kati ya Shilingi 100,000 hadi 200,000 kwa mtu mmoja, huku meza ya watu 10 ikigharimu Shilingi milioni Mbili (2) Tiketi za tamasha hili zinapatikana kupitia Nilipe App.
Katika tamasha hilo, waimbaji mbalimbali watahudumu akiwemo mwimbaji maarufu kutoka Nigeria Mercy Chinwo, pamoja na waimbaji wa hapa nyumbani wakiwemo Boaz Danken, Rehema Simfukwe, Joel Lwaga, na Neema Gospel.
Tamasha la pili ambalo ndilo la vijana, litafanyika kama ilivyo desturi katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe Juni 21, 2025 kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni. Kiingilio katika tamasha hili kitakuwa Shilingi 5,000 na tiketi tayari zinapatikana.
Ameeleza kuwa Kwa miaka 12 mfululizo, tamasha la Twen’zetu kwa Yesu limekuwa jukwaa muhimu kwa vijana kujifunza, kuabudu, na kujijenga kiroho. Takwimu zinaonesha kuwa takribani vijana 35,000 wamekuwa wakihudhuria kila mwaka katika matamasha haya.
Kauli mbiu ya tamasha la mwaka huu ni “Ishi kwa Malengo”, ikilenga kuhamasisha vijana kuishi kwa maono na kuwa na mwelekeo sahihi katika maisha yao. Kauli mbiu hiyo inasisitiza mafundisho kutoka Mithali 29:18a: “Pasipo maono, watu huacha kujizuia.”
Kuelekea kilele cha tamasha la Kawe, kutafanyika matamasha ya utangulizi katika Sharika za KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani kuanzia Jumapili ya Aprili 27, 2025.
Mnenaji mkuu wa mwaka huu atakuwa Askofu Lawi Mwankuga wa Kanisa la Morovian Jimbo la Mashariki – Dar es Salaam.
Kwa mara nyingine, tamasha hili linaloandaliwa na Upendo Media linalenga kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu kupitia mafundisho, uimbaji, na ushirikiano wa kiimani kwa lengo la kujenga taifa lenye nidhamu, uwajibikaji na uzalendo.