Katika hatua inayochochea matumaini mapya kwa wakazi wa vijijini, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Rashid Kawawa, amekabidhi rasmi gari jipya la wagonjwa kwa wananchi wa Kata ya Magazini, Hafla hiyo ya makabidhiano imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wananchi waliojitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Gari hilo la wagonjwa la kisasa ambalo limetolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya chini ya Waziri Jenista Mhagama, litatumika kutoa huduma za dharura kwa zaidi ya vijiji vinne vilivyopo katika Kata ya Magazini, Vijiji hivyo ni pamoja na Magazini, Sasawala, Amani na Likusanguse maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya usafiri wa haraka kwa wagonjwa.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Kawawa alieleza kuwa kupatikana kwa gari hilo ni matokeo ya juhudi za muda mrefu alizozifanya kwa kushirikiana na serikali, kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaboreshwa hasa katika maeneo ya vijijini. “Hatimaye juhudi zetu zimezaa matunda. Kwa muda mrefu nimekuwa nikiwasiliana na serikali ili kuhakikisha wananchi wa Jimbo la Namtumbo wanapata gari la wagonjwa, na sasa tunaona matokeo yake,” alisema kwa furaha kubwa.
Aidha, Mbunge huyo hakusita kumpongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kwa kulisikia kilio cha wananchi wa Namtumbo na kulipa uzito unaostahili, Alieleza kuwa upatikanaji wa gari hilo si tu kwamba utaokoa maisha ya wananchi bali pia utaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya.
Wananchi waliokuwepo katika hafla hiyo walionekana kufurahishwa na hatua hiyo, wakimpongeza Mbunge wao kwa juhudi zake zisizokoma na kumuunga mkono Rais Samia kwa dhamira yake ya dhati katika kuboresha maisha ya Watanzania wote, Walisema kuwa kabla ya ujio wa gari hilo walilazimika kutumia pikipiki au magari ya kukodi kusafirisha wagonjwa hali iliyowekea maisha yao hatarini.
Makabidhiano haya yanatajwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa mkakati mpana wa serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za kijamii hususan katika sekta ya afya Kwa mara nyingine serikali imeonesha dhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi maendeleo, hususan wale wa maeneo ya pembezoni ambao mara nyingi husahaulika.
Kwa upatikanaji wa gari hili la wagonjwa, matumaini ya huduma bora za afya kwa wananchi wa Kata ya Magazini sasa yamechomoza upya, Ni hatua inayothibitisha kuwa serikali sikivu ni ile inayosikiliza kilio cha wananchi wake na kuchukua hatua za dhati kuleta suluhisho la kudumu.