NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO
WAZIRI wa Ujenzi, Mhandisi Abdallah Ulega, ametembelea na kukagua barabara ya Malinyi mkoani Morogoro ambayo imeharibika kutokana na maji ya Mto Furuwa kuvunja kingo na kupita juu ya barabara, hali iliyosababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya kijiji cha Misegese na Malinyi mjini.
Ziara hiyo ya siku moja imefanyika kufuatia malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Misegese ambao wamekuwa wakikosa huduma muhimu za kijamii kutokana na barabara hiyo kutopitika kila msimu wa mvua.
Akizungumza mara baada ya kukagua eneo la Mwembeni, Waziri Ulega amesema serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 18 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja ya kudumu yatakayosaidia kutatua changamoto ya kukatika kwa mawasiliano katika eneo hilo.
“Tumeona hali halisi ilivyo. Serikali imelidhia kutoa fedha hizi ili kuhakikisha kuwa wananchi wa maeneo haya hawapati tena tabu wakati wa mvua,” alisema Waziri Ulega.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alimshukuru Waziri Ulega kwa kufika na kujionea tatizo hilo, huku akiahidi kuweka mikakati ya ulinzi kwa barabara hiyo mara baada ya matengenezo kukamilika.
“Nawashukuru sana TANROADS Pamoja na TARURA kwa ushirikiano tangu tatizo hili lilipojitokeza. Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Wilaya itaweka ulinzi wa kutosha kuhakikisha kuwa shughuli za kilimo hazifanyiki kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara na vyanzo vya maji,” alisema Malima.
Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Mhe. Antepas Mgungusi, alisema wananchi wa Misegese wanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na huduma nyingi muhimu kupatikana upande wa pili wa mto, yaani Malinyi mjini.
Naye Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro,Mhandisi Emmanuel Ndyamukama, alisema timu ya wataalam imeweka kambi kwenye maeneo yote yenye changamoto ili kuhakikisha kuwa mawasiliano yanarejeshwa haraka iwezekanavyo.
Waziri Ulega amekuwa mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya barabara iliyoharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko maeneo mbalimbali ya mkoa huo.