Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua rasmi kampeni ya kitaifa ijulikanayo kama “Toboa Kidijitali”, ambayo inalenga kuhamasisha wananchi kutumia mifumo ya kisasa ya miamala ya kifedha kwa njia ya kidijiti, sambamba na kuwazawadia wateja wake wanaoshiriki kikamilifu katika matumizi ya huduma hizo.
Uzinduzi huo umefanyika siku ya Ijumaa Aprili 25, 2025, Makao Makuu ya TCB yaliyopo eneo la Makumbusho, jijini Dar es Salaam, ukihudhuriwa na wadau mbalimbali wa benki, wafanyakazi, wateja, pamoja na wawakilishi wa vyombo vya habari.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Mihayo, Mkurugenzi wa Wateja Binafsi na Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati, Bi. Lilian Mtali, amesema kuwa benki hiyo imeamua kuwekeza zaidi ya shilingi milioni 200 katika kampeni hii kama sehemu ya kurudisha kwa jamii, lakini pia kama njia ya kuendelea kukuza matumizi ya teknolojia ya kifedha nchini.
“Hii ni namna ya kuwarudishia wateja wetu, jamii na wafanyabiashara wadogo wanaotuzunguka. Tumepanga kuwazawadia washindi mbalimbali watakaoibuka kidedea kupitia miamala wanayofanya kwa njia ya kidijiti kwa kipindi cha miezi minne,” amesema Mtali.
Ameongeza kuwa TCB imekuwa mstari wa mbele katika kuwekeza kwenye ubunifu wa mifumo ya huduma za kifedha ili kumwezesha Mtanzania kufanya miamala kwa haraka, kwa usalama na mahali popote, bila kulazimika kufika tawi la benki.
“Kwa kutumia huduma kama Popote Mobile App, Popote Visa Card, na mfumo wa Lipa Popote, mteja anaweza kufanya miamala bila usumbufu. Tunasisitiza uhuru wa kujihudumia kibenki kwa kutumia teknolojia kwa sababu muda ni pesa,” amesema Mtali.
Kwa upande wake, Jesse Jackson, Afisa Mkuu wa Huduma za Kidijiti na Ubunifu wa TCB, amesema kuwa kupitia kampeni ya Toboa Kidijitali, benki hiyo inatarajia kutoa zawadi mbalimbali kwa washindi, ikiwemo gari aina ya Mazda, simu ya iPhone 16 Pro Max, bajaji, bodaboda kila mwezi kwa kipindi cha miezi minne.
Jackson amesema kuwa kampeni hii inalenga si tu kuongeza miamala ya kidijitali, bali pia kuchochea ujumuishi wa kifedha kwa makundi yote ya Watanzania, wakiwemo wale wa vijijini na maeneo ya pembezoni.
“Kwenye miaka mitano iliyopita, sekta ya kibenki imepata mageuzi makubwa. Mwaka 2020 tulikuwa na miamala ya kidijiti milioni 14, lakini mwaka jana idadi hiyo ilifikia milioni 21, ongezeko la asilimia 45. Hili linaonesha kuwa tuko kwenye njia sahihi, lakini bado kuna fursa kubwa ya kufanya vizuri zaidi,” amesema Jesse.
Ameeleza kuwa licha ya mafanikio hayo, bado sehemu kubwa ya Watanzania hutegemea fedha taslimu kwa miamala yao ya kila siku, hivyo kuna haja ya kuongeza elimu na kutoa motisha kama hii ili kuongeza matumizi ya miamala ya kisasa.
Kampeni ya Toboa Kidijitali imelenga kuhamasisha matumizi ya huduma za kidijiti za benki, ktoa zawadi kwa washiriki wa kampeni kama motisha, kuchangia katika ujumuishi wa kifedha nchini Tanzania na kupunguza utegemezi wa fedha taslimu (cash economy).
Benki ya Biashara Tanzania (TCB) ni benki ya umma inayolenga kutoa huduma jumuishi kwa Watanzania wote. Kupitia kampeni mbalimbali za ubunifu kama “Toboa Kidijitali,” TCB inaendelea kujiimarisha kama kinara wa huduma za kifedha zinazowafikia watu wengi kwa njia rahisi na ya kisasa.