Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kesho, Aprili 26, wananchi wametakiwa kuuenzi Muungano huo kwa kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani na mshikamano uliodumu tangu enzi za mababu, hadi kizazi cha sasa na kijacho.
Wito huo umetolewa leo Aprili 25 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea, Mtela Mwampamba, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Songea, wakati wa shughuli ya usafi katika Shule ya Sekondari Ruhuwiko, iliyopo Kata ya Ruhuwiko, Manispaa ya Songea. Shughuli hiyo iliratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea.
Mwampamba amewasisitiza Watanzania kuendelea kushikamana na kuuenzi Muungano kwa vitendo, akieleza kuwa kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), asilimia 94 ya Watanzania wa sasa wamezaliwa wakati wa Muungano, huku asilimia 6 pekee wakiwa wamezaliwa kabla ya Muungano.
Amesema kwa kuzingatia hilo, ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha anadumisha na kuendeleza Muungano kwa vitendo. Amesisitiza kuwa kazi ya usafi iliyofanyika ni sehemu ya kuadhimisha Muungano, sambamba na maandalizi ya uwekaji wa jiwe la msingi katika shule hiyo mpya, unaotarajiwa kufanywa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Sadiki Said Mrisho, mmoja wa maafisa wa Manispaa hiyo ameeleza kuwa shughuli ya usafi ni utekelezaji wa maagizo ya serikali kuhakikisha maeneo ya huduma kwa jamii yanawekwa katika hali ya usafi na ustaarabu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea maadhimisho ya Muungano.
Ameeleza kuwa serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo, ambayo inatarajiwa kuwa suluhisho kwa changamoto ya wanafunzi wa Kata ya Ruhuwiko ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwenda shule zilizoko katika kata jirani.
Kwa mara ya kwanza, Kata ya Ruhuwiko itakuwa na shule yake ya sekondari ya kujitegemea, hatua ambayo imepokelewa kwa furaha na shukrani kubwa kutoka kwa wananchi wa eneo hilo. Wananchi hao wamesema kuwa ujio wa shule hiyo utarahisisha upatikanaji wa elimu kwa watoto wao na hivyo kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Maadhimisho ya Muungano katika Wilaya ya Songea yalianza rasmi Aprili 17 kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutembelea watoto yatima na kufanya usafi. Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufikia kilele kesho, Aprili 26, kwa maandamano ya amani katika maeneo mbalimbali ya Songea Mjini, yatakayofuatiwa na mdahalo maalum kuhusu Muungano wa Tanzania.