NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa kuboresha mifumo yake ya usajili wa biashara kwa kutumia teknolojia ya kidigitali, hatua inayorahisisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wadau mbalimbali. Pongezi hizo alizitoa leo, Aprili 25, 2025, alipofanya ziara ya kikazi kutembelea Ofisi za Makao Makuu ya BRELA jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Dkt. Serera alijionea jinsi kazi za BRELA zinavyofanyika na kutoa maelekezo kuhusu namna Wizara inavyoweza kusaidia taasisi hiyo katika kutimiza majukumu yake kwa kiwango cha kitaifa na kimataifa, hususan katika kurahisisha shughuli za kibiashara nchini.
“Nimeona ushirikiano mkubwa sana, lakini jambo kuu lililosababisha kazi zifanyike ni suala la ubunifu. Ubunifu umefanya kazi za BRELA kufanikiwa, na tumeona mabadiliko makubwa. Mfano, wakati fulani ufunguzi wa kampuni ulichukua muda mrefu hadi miezi, lakini sasa hivi, ukikamilisha nyaraka zako, unaweza kufungua kampuni yako ndani ya siku moja,” alisema Dkt. Serera.
Aidha, Dkt. Serera alisisitiza umuhimu wa kutumia mtandao katika utoaji wa huduma za usajili ili kuendana na kasi ya teknolojia inayokua. Alieleza kuwa njia hii itasaidia pia kuondokana na mlundikano wa leseni zinazotolewa na taasisi nyingine ambazo pia zinahusika na utoaji wa leseni za biashara.
“Tunaelewa kuwa taasisi yetu imepewa dhamana ya kuanzisha na kutoa leseni mbalimbali. Hata hivyo, zipo taasisi nyingine zinazoruhusiwa kutoa leseni. Lakini BRELA, ambayo miundombinu yake imewekwa vizuri, ni vyema ikaachiwa jukumu hili. Tukiweza kuhusianisha vyema, tutaboresha zaidi utoaji wa leseni na kuondokana na changamoto za mlundikano wa leseni na ada zinazolipwa,” alisisitiza Dkt. Serera.
Katika hatua nyingine, Dkt. Serera ameitaka BRELA kulipa kipaumbele kundi maalum la kina mama na vijana walioanzisha biashara changa ili kurahisisha mazingira ya kusajili kampuni kwa kuweka utaratibu mahsusi utako wasaidia wajasiriamali hawa na kuondoa vikwazo kwao.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, alitoa shukrani kwa Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Suleiman Serera, na kuahidi kuwa atatekeleza msisitizo aliouweka kuhusu matumizi ya teknolojia. Bw. Nyaisa alisema kuwa BRELA itaendelea kuendana na ukuaji wa teknolojia mpya, hasa matumizi ya akili mnemba, ili kuendana na mahitaji ya soko na kuepuka kubaki nyuma ya wakati.
Alisisitiza pia umuhimu wa nidhamu kwa watumishi wa taasisi, akieleza kuwa kila mtumishi wa umma anapaswa kutambua jukumu lake na kulinda maslahi ya serikali.
“Nidhamu katika utendaji ni jambo la msingi sana. Taasisi ya BRELA ni muhimu kwa sababu ndio lango kuu la wafanyabiashara na wawekezaji wengi. Ufunguzi wa makampuni unahusisha mambo mengi, na kuna watu wenye nia njema ya kufanya biashara, lakini pia wapo wanaotaka kutumia kampuni kwa madhumuni ya kuhujumu. Hivyo, nidhamu ni muhimu sana,” alisisitiza Bw. Nyaisa.
