Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile, amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa vitendo, akisisitiza kuwa ni matokeo ya jitihada kubwa za waasisi wa Taifa ambazo hazipaswi kupuuzwa.
Akizungumza leo Aprili 26, 2025, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano, Ndile aliwataka Watanzania wote kuwa walinzi wa amani na mshikamano, huku akilaani vikali vitendo vya kuchochea migawanyiko au kuvuruga utulivu wa Taifa.
Katika tukio hilo lililohusisha riadha ya pamoja kati ya watumishi wa umma na baadhi ya wananchi wa Songea, DC Ndile alisisitiza kuwa umoja wa kitaifa ndiyo nguzo ya mafanikio, akitoa mfano wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kama daraja la kuunganisha makabila mbalimbali nchini.
Ameeleza kuwa nchi nyingi duniani zimesambaratika kutokana na kukosekana kwa mshikamano, lakini Watanzania wameendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa wamoja licha ya tofauti zao, na kwamba jukumu la kulinda hali hiyo ni la kila mmoja.
Ndile amesema shughuli za maadhimisho zilianza kwa kufanya usafi katika taasisi mbalimbali na leo zimehitimishwa kwa mbio za riadha zilizoambatana na ujumbe wa mshikamano, ambapo watu zaidi ya 350 walishiriki.
Amehimiza umuhimu wa mazoezi ya mwili kama sehemu ya kujenga afya bora kwa Watanzania na jamii imara, akiwataka wananchi kuanzisha tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kupunguza gharama za matibabu na kuimarisha ustawi wa maisha yao.
Katika salamu zake kwa madereva, aliwataka kuzingatia nidhamu barabarani kwa kuwapa heshima watembea kwa miguu na wale wanaofanya mazoezi, akisema barabara ni za wote na zinapaswa kuwa sehemu salama kwa kila mtumiaji.
Akihitimisha hotuba yake, DC Ndile aliwahimiza viongozi wa taasisi zote kuendeleza ushirikiano na wananchi katika shughuli mbalimbali za kijamii, ili kuimarisha mshikamano, amani na maendeleo ya pamoja kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.