Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Hemed Challe, amesema kuelekea uchaguzi wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi ni jambo la kawaida kuwa na makundi tofauti tofauti ya wanaowania nafasi mbalimbali, lakini baada ya mchakato huo ni lazima wanachama wote waungane na kuwa kitu kimoja kwa ajili ya maslahi ya chama na taifa kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa chama hakihitaji kuona siasa za kuchukiana, matusi au kutupiana maneno machafu bali siasa za kistaarabu zitakazowajenga viongozi na kuwashawishi wananchi kwa hoja, si kwa mabavu au mivutano isiyo na tija. Amesema hakuna sababu ya kuchukiana kwa sababu ya siasa, kwani ushindani ni wa muda na demokrasia inaruhusu tofauti za mawazo.
Hemed amewakumbusha viongozi kuwa dhamana waliyonayo ni matokeo ya uamuzi wa wananchi, na ni wananchi hao hao watakaofanya uamuzi kama waendelee au wasiendelee kuwaweka kwenye nyadhifa hizo. Ameeleza kuwa katika siasa ni jambo la kawaida kuchaguliwa leo na baadae kuachwa, hivyo hakuna sababu ya kupandwa na hasira au hofu.
Aidha, amesema uimara wa CCM umetokana na kuzingatia misingi ya kidemokrasia na kufuata taratibu zake, ikiwemo kurudi kwa wananchi kila baada ya miaka mitano ili kuomba ridhaa upya. Hii ndiyo sababu Chama kimeendelea kuwa imara na kuaminiwa na wananchi wengi.
Katika hatua nyingine, Hemed amewahakikishia wanachama wote wa CCM kuwa msimamo wa chama ni kuhakikisha haki inatendeka kwa kila mmoja, na hakuna mwanachama anayepaswa kuogopa au kuzuiwa kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya udiwani au ubunge. Amesema chama kitachukua hatua kwa yeyote atakayejaribu kukwamisha au kutisha wagombea kabla hata ya mchakato kuanza rasmi.
Ameeleza kuwa kila Mtanzania ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kujitathmini na kama anaona anaweza kuwa kiongozi, basi ajitokeze kuchukua fomu pindi wakati ukifika. Kwa wale ambao hawana nia ya kugombea, wanapaswa kuitumia haki yao ya kikatiba kwa kuchagua viongozi wanaoamini watawaletea maendeleo.
Katika kuunga mkono jitihada za chama, MNEC Hemed Challe ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi za CCM katika Kata za Mjimwema na Matarawe, ambapo alichangia kiasi cha shilingi milioni moja moja kwa kila ofisi, ili kusaidia kukamilisha ujenzi huo kama ulivyopangwa.
Wananchi waliokuwa wakihudhuria mikutano hiyo katika maeneo mbalimbali wamempongeza kwa kazi nzuri na moyo wa kujitolea alioonesha. Wamesema wako tayari kuendelea kushirikiana na CCM kutokana na kazi kubwa inayofanywa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Kwa sasa, wamesema hawana madai kwa Rais bali wao ndio wako kwenye deni la kumpigia kura kwa kishindo ifikapo Oktoba.
Hemed Challe ameanza ziara ya siku tatu katika Manispaa ya Songea kuanzia Aprili 26 hadi Aprili 28, ambapo leo ametembelea na kufanya mikutano katika maeneo ya Ruhuwiko ukiwajumuisha wakazi wa Kata ya Ruhuwiko, Mwengemshindo na Lilambo, na kuhitimisha siku yake kwa mkutano mkubwa uliofanyika katika shule ya Msingi Kiblang’oma, uliowakutanisha wakazi wa Kata za Lizaboni, Matarawe na Mjimwema.
Katika ziara hiyo, aliwataka viongozi wa ngazi za chini ndani ya CCM kuendeleza mshikamano na kushirikiana kwa karibu na wanachama katika kuimarisha chama, Alisisitiza umuhimu wa mawasiliano bora na uwazi baina ya viongozi na wanachama, ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa na uelewa sawa wa masuala ya chama na maendeleo ya jamii, Pia aliwataka viongozi kuwa mfano wa kuigwa kwa kuzingatia maadili, uwajibikaji na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.