Na Mwandishi wetu, Singida
Katika kuadhimisha Wiki ya Maonesho ya Kitaifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Benki ya NMB imedhamini na kushiriki bonanza maalum lililoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) mjini Singida.
Bonanza hilo, lililofanyika katika Uwanja wa VETA – Singida, lilikutanisha makampuni kutoka sekta binafsi na ya umma yaliyoshindana katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete na kuvuta kamba, likiwa na lengo la kuhimiza afya na usalama kazini kupitia michezo.
Mgeni rasmi katika hafla hii alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, ambaye aliipongeza Benki ya NMB kwa mchango wake mkubwa katika kufanikisha tukio hilo muhimu. Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mhe. Dendego alisisitiza umuhimu wa mazoezi katika kuboresha afya za wafanyakazi, akieleza kuwa ustawi wa wafanyakazi ni msingi wa uzalishaji bora na maendeleo ya taifa.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ni “Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia za Kidijitali katika Kuimarisha Usalama na Afya Mahali Pa Kazi,” ikilenga kuhimiza matumizi ya teknolojia na ubunifu wa kidijitali katika kulinda afya na usalama wa wafanyakazi.
Mbali na kushiriki katika bonanza, Benki ya NMB pia imeweka banda maalum katika Viwanja vya Maonesho vya Mandewa ambapo wananchi wanapata fursa ya kujifunza namna benki hiyo inavyohakikisha usalama mahali pa kazi, pamoja na kupata elimu ya kifedha na huduma nyingine za kibenki.