

MKUU wa Mkoa wa Singida( RC) Mheshimiwa Halima Dendego ameisifu kampuni ya kuchimba dhahabu ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kuzingatia usawa wa wanawake katika utendaji wake kazi wenye tija kwa tifa.
Akizungmza baada ya kutembelea banda la GGML katika Maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani yanayoendelea Kitaifa mkoani Singida, RC Dendego amesema kampuni ya GGML imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya madini na kuchangia ukuaji uchumi wa taifa kupitia uwekezaji ilioufanya.
“ Nimefurahishwa sana kuona mpangilio mzuri wa mabanda mbalimbali katika maonesho haya,”
“Kipekee nimevutiwa na ushiriki mzuri wa mgodi wa GGML, ambapo mbali na kuwa na vifaa vya kisasa vya kulinda usalama wa kazi sehemu za kazi, pia nimeona namna mnavyozingatia usawa wa kijinsia kwa kuja na watalaamu mbalimbali wa jinsia zote wanawake na wanaume wakielezea maeneo mbalimbali ya utendaji kazi wenu namna mlivyowekeza katika kutumia akili mnemba kulinda usalama mahali pa kazi,”
“ Na hii inaonesha ni namna gani mnazingatia usawa wa kijinsia katika kutoa fursa kwa jinsia zote,” amesema .
Amesema kuwa amefarijika sana kuwaona GGML katika mkoa wa Singida na wanakaribishwa sana katika uwekezaji wa maeneo mbalimbali mkoani humo,”
“Jina lenu ni kubwa sana hapa Singida na mnajulikana kila kona kwa kazi yenu mzuri mnayoifanya,”amesema RC Dendego na kuongeza ;
Awali, akimkaribisha RC Dendego katika banda hilo, Mtaalamu wa Afya na Usalama wa GGML Bw. Volentine William amesema kuwa wameamua kushiriki maonesho hayo ili kuwapa fursa wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani kujifunza kazi mbalimbali zinazofanywa na mgodi huo mkubwa hapa nchini.
Akielezea kuhusu umuhimu wa kuzingatia usalama wa wafanyakazi katika maeneo mbalimbali ya mgodi huo ikiwemo kwa jamii zinazouzunguka, Bw.Volentino amesema kuwa mgodi huo umewekeza vya kutosha katika ununuzi wa vifaa vya kisasa ili kulinda usalama wa wafanyakazi kwa kutumia akili mnemba (AI).
“Tuna vifaa mbalimbali kama vile ndege zisizotumia rubani (drone) ambazo zinauwezo wa kuingia chini ya ardhi na kutoa tahadhari ya hatari inayoweza kutokea,”
“Lakini pia tuna mitambo ya kisasa inayotumia povu linalotokana na mbolea kwa ajili ya kuzimia moto pindi janga linapotokea bila kuathiri mazingiza,” amesema Bw. William.
Pia amesema kuwa mgodi wa GGML, ambao unajivunia kuwa kinara wa tuzo ya usalama duniani kwa miaka minne mfululizo ( Global Safety Award) , pia umekuwa ukishiriki katika kusaidia maendeleo ya jamii ikiwemo ujenzi wa takriban madarasa 100 pamoja na zaidi ya zahanati na vituo vya afya 50 ili kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Lakini pia imekuwa ikitoa msaada wa fedha kupitia mpango unaoitwa ‘Kili Challenge’ kwa ajili ya kuwasaidia watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) ili kuwasaidia kuwa na afya njema na kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa taifa.
Mgodi wa GGML umekuwa ukichukua jitihada mbalimbali za kuwahamasisha wanawake kuwa sehemu ya mgodi huo pale fursa zinapotokea na sehemu kubwa ya wanawake wanafanyakazi katika nafasi mbalimbali za mgodi huo.
Jitihada hizi zinatokana na uwepo wa program maalum za kuwajengea uwezo wanawake katika mgodi huo, ambayo imewezesha wanawake kushika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo ngazi ya umeneja.