Na Issa Mwadangala.
Watoto walio wengi hufanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji na hivyo kupelekea kushindwa kufurahia utoto wao na kuwaletea madhara makubwa kimwili na kiakili.
Hayo yalisemwa Aprili 26, 2025 na Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Akama Shaaban akiwa ameambatana na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Eletisia Mtweve ambaye ni Kaimu Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Songwe walipotembelea Kituo cha Radio cha Vwawa 103.7 iliyopo Mbozi Songwe.
“‘Sisi Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na taasisi nyingine tunao wajibu mkubwa wa kuelimisha jamii ili kukomesha vitendo hivi pamoja na kuhamasisha jamii juu ya ulinzi wa mtoto na kuchangia katika kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya watoto” alisema ACP Akama.
Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Eletisia Mtweve amewataka wananchi wa Mkoa wa Songwe kuendelea kulinda haki za Watoto ikiwemo haki ya kuwaendeleza kielimu, wazazi kuendelea kuwalea Watoto katika misingi ya kiimani pamoja na kiutamaduni ili wawe na maadili mema na kujifunza kusaidia kazi za nyumbani ambazo haziathiri masomo.
Mwisho alimalizia ACP Akama kwa kuitaka jamii kwa ujumla kuachana na mila potofu, ambazo zinasababisha kuwafanyia ukatili watoto jambo ambalo linachangia kurudisha nyuma maendeleo ya ukuaji wao.