Serikali kupitia Wizara ya Madini imetunga kanuni za msaada wa kiufundi katika Leseni ndogo za uchimbaji wa Madini ambapo zitaratibu ushiriki wa wageni katika Leseni ndogo za uchimbaji wa Madini(PML) ambazo kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha Sheria ya Madini sura ya 123,kimezitamka Leseni hizi kama maalum kwa ajili ya Watanzania.
Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Madini kinatoa ruhusa kwa mmiliki wa Leseni ndogo ya uchimbaji madini kuingia ubia na mgeni kwa makubaliano ya msaada wa kiufundi(𝙏𝙚𝙘𝙝𝙣𝙞𝙘𝙖𝙡 𝙎𝙪𝙥𝙥𝙤𝙧𝙩).
Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka 2024/25 Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde alisema Serikali inatarajia kutunga kanuni za kuratibu ushiriki wa wageni katika Leseni ndogo kwa kuwa kumejitokea wimbi kubwa la wageni kuingia katika maeneo ya wachimbaji wadogo kwa mgongo wa “Msaada wa Kiufundi”ambao haukuwa na utaratibu mzuri na hivyo kupelekea wachimbaji wengi wadogo kutopata manufaa yaliyokusudiwa ya kujiimarisha kupitia Leseni ndogo za uchimbaji na wakati mwingine katika vikundi vya wachimbaji viongozi wachache kuingia makubaliano ya msaada wa kiufundi bila kushirikisha wahusika wote na hivyo kuzua migogoro isiyo na sababu.
Tarehe 25.04.2025 limetolewa Tangazo la Serikali Na. 260 kuitambulisha kanuni hii mpya kuanza utekelezaji wake ikiwa ni ahadi iliyotolewa na Waziri Mavunde akitekeleza maelekezo ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan.
Kanuni hiyo imetaja mambo mengi muhimu,yakiwemo;
1. Usajili wa Mikataba ya Kiufundi kwenye Tume ya Madini baina ya Mchimbaji Mdogo na Mtoa Msaada wa kiufundi.
2. Kufafanua maana ya maneno “Msaada wa Kiufundi” ili kutimiza lengo mahsusi la kuongeza tija ya uzalishaji na kukuza ujuzi.
3. Mgawanyo wa Mapato kati ya Mwenye Leseni Ndogo na Mtoa msaada wa Kiufundi kwa madini yatakayozalishwa.