Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yameiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa za kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya Anga.
Amesema hayo leo Jumatatu (Aprili 28, 2015) wakati alipofungua Mkutano wa 73 wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege kwa Ukanda wa Afrika (ACI Afrika) unaofanyika kwenye Hotel ya Mount Meru.
Amesema kuwa moja ya eneo ambalo Rais Dkt. Samia ameendelea kusimamia ni ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege nchini ikiwemo ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha msalato kilichopo jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia anaendelea na uboreshaji wa viwanja vingine vya kimkakati vya Kilimanjaro, Unguja, Pemba, Mwanza, Kigoma, Tabora, Shinyanga na Sumbawanga. “Pia tunaendeleza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti unaolenga kukuza utalii wa mazingira huku tukihifadhi mfumo ikolojia wa Serengeti”.
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imewekeza katika ununuzi wa vifaa vya kisasa vya mawasiliano kwenye viwanja wa ndege na masafa marefu ili kuhakikisha kunakuwa na usalama wa ndege na abiria.
Amesema kuwa kutokana na jitihada mbalimbali za Serikali za kuiimarisha Sekta ya anga, Tanzania imetajwa na Shirika la ICAO kushika nafasi ya nne barani Afrika kwenye masuala ya usalama wa anga
Kadhalika Uwanja wetu wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere umefanikiwa kushinda Tuzo ya Usalama ya Baraza la Viwanja vya Ndege Duniani, katika viwanja vyenye miruko ya ndege 50000 kwa mwaka”
Akizungumzia kuhusu shirika la ndege la Tanzania (ATCL) Waziri Mkuu amesema hivi sasa ndege zake zinatoa huduma ya usafiri katika viwanja 15 vya ndani na nje ya nchi katika nchi za Dubai, Mumbai, Guangzhou, Johannesburg, Nairobi, Harare, Lusaka, Entebe na Kinshasa
“Shirika pia linatarajia kuongea safari zake katika miji ya London, Lagos, Accra, Juba, Muscat na maeneo mengine ya masoko ya kimkakati ili kuiunganisha Tanzania Kikanda na Kimataifa”
Kwa Upande wake, Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa mkutano huo inatoa jukwaa adimu linalowaleta pamoja viongozi na wasimamizi wa usafiri wa anga, waendeshaji wa viwanja vya ndege kujadili na kubadilishana mawazo katika kuboresha na kuikuza sekta ya usafiri wa Anga.
Naye Rais wa Baraza la Viwanja vya Ndege Afrika Emmanuel Chaves amesema kuwa sio tu kwenye utungaji wa Sera bali kwenye maamuzi tunayoyafanya sasa katika kushirikiana “Kama tutaamua kwa dhati tutajenga Afrika yenye muunganiko na ushindani katika sekta ya anga”
Pia Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo ametoa shukrani kwa wadau mbalimbali waliofika katika mkutano huo wenye tija hasa katika ukanda wa Afrika.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia wadau mbalimbali wa viwanja vya ndege wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 73 wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege kwa Ukanda wa Afrika (ACI Afrika) unaofanyika jijini Arusha
Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa akziungumza kuhusu jukwaa hilo adimu linalowaleta pamoja viongozi na wasimamizi wa usafiri wa anga, waendeshaji wa viwanja vya ndege kujadili na kubadilishana mawazo katika kuboresha na kuikuza sekta ya usafiri wa Anga.
Rais wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege kwa Ukanda wa Afrika (ACI Afrika) Emanuel Chaves akizungumzia mafanikio endelevu sekta ya anga afrika wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 73 wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege kwa Ukanda wa Afrika (ACI Afrika) unaofanyika jijini Arusha
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara akizungumzia mipango mbalimbali ya wizara katika kukuza usafiri wa Anga hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo akizungumzia fursa mbalimbali zilizopo kwenye viwanja vya ndege wakati wa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 73 wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege kwa Ukanda wa Afrika (ACI Afrika) unaofanyika jijini Arusha.
Picha ya pamoja