Serikali imetoa wito kwa waajiri, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kujenga utamaduni wa kujikinga dhidi ya ajali na magonjwa mahali pa kazi ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza katika uchumi na ustawi wa wafanyakazi nchini.
Wito huo wa Serikali umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, alipowaongoza mamia ya Watanzania kuadhimisha siku ya usalama na afya mahali pa kazi duniani ambayo imeadhimishwa Kitaifa Mkoani Singida katika Viwanja vya Maadhimisho Mandewa-Singida Mjini.
Akiwahutubia katika kilele cha maadhimisho hayo, Waziri Kikwete, amesema serikali inatambua umuhimu wa kulinda nguvukazi yake hivyo imeendelea kuiwezesha Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
“Rais wetu Mhe, Samia Suluhu Hassan, anatambua na kujali afya na usalama wa wafanyakazi nchini na amethibitisha hilo kwa vitendo kupitia uwezeshaji ambao amekuwa akiufanya kwa Taasisi yetu ya OSHA hususan kwa kuipatia vitendea kazi na kuwaongezea watumishi ili kuongezea uwezo wa kuwahudumia Watanzania,” amesema Mhe. Kikwete na kuongeza:
“Kadhalika serikali imechukua hatua mahsusi kuimarisha usalama wa wafanyakazi katika miradi ya kimkakati ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR), Barabara za Mwendokasi Jijini Dar es Salaam, Mradi wa Bwawa la Mwl. Nyerere na mingine mingi kwa kuhakikisha uwepo wa Maafisa Usalama na Afya, kutoa mafunzo ya mara kwa mara pamoja na kuwapatia vifaa kinga stahiki.”
Aidha, Waziri Kikwete amesema serikali imeanza kuchukua hatua kuandaa sera zinazowajumuisha wajasiriamali wadogo katika fursa mbalimbali kiuchumi yakiwemo masuala ya usalama na afya kazini ambapo Taasisi ya OSHA imeanzisha program maalum ijulikanayo Afya Yangu-Mtaji Wangu inayowezesha kuyatambua makundi ya wajasiriamali wadogo na kuyawezesha kufanya shughuli zao kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya kazini.
Akiizungumzia Kauli Mbiu ya Maadhimisho kwa mwaka huu isemayo: “Nafasi ya Akili Mnemba na Teknolojia za Kidijitali katika Kuimarisha Usalama na Afya Mahali pa Kazi”, Kikwete amesema teknolojia ina mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi wa utendaji ambapo amewashauri waajiri kujiweka tayari kupokea mabadiliko ya teknolojia huku wakichukua tahadhari dhidi ya athari hasi za teknolojia ikiwemo kuhatarisha baadhi ya fursa za ajira kupotea.
Awali, akitoa salamu zake kwa hadhira iliyohudhuria maadhimisho, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema maadhimisho yanalenga kuhamasisha uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya mahali pa kazi nchini ambapo Taasisi yake huratibu maadhimisho hayo kwa niaba ya Serikali kwa kushirikiana na wadau wa utatu ambao ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wakishauriwa kwa karibu na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Ameanisha shughuli ambazo ni sehemu ya maadhimisho ya mwaka huu kuwa ni pamoja na maonesho ya usalama na afya mahali pa kazi, kliniki ya uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, shindano la tuzo za usalama na afya mahali pa kazi, bonanza la michezo pamoja na mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo.
Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Masharika, Bi. Caroline Khamati Mgalla, ameipongeza Serikali ya Tanzania na wadau wa usalama na afya nchini kwa maandalizi mazuri ambayo yamehusisha shughuli zenye tija kwa jamii zikiwemo huduma ya upimaji afya na matibabu kwa wananchi na mafunzo kwa wajasiriamali wadogo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Bi. Suzanne Ndomba-Doran amewapongeza waajiri kwa mwitikio mzuri katika maadhimisho ya mwaka huu huku akiwashauri kutumia tekenolojia mbali mbali ikiwemo Akili Unde ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji.
Rais wa TUCTA, Bw. Tumaini Nyamhokya ametoa tahadhari kwa waajiri nchini kuhakikisha kwamba teknolojia mpya zinazotumika katika uzalishaji haziathiri ajira za Watanzania.
Tarehe 28, Aprili kila mwaka hutambulika Kimataifa kama siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ambapo Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku hiyo. Lengo la maadhimisho haya ni kuhamasisha uwepo wa mazingira salama na yenye kulinda afya za wafanyakazi katika sehemu za kazi pamoja na kuwakumbuka wafanyakazi walioumia au kupoteza maisha wakiwa wanatekeleza majukumu yao.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Tumaini Nyamhokya akiwasilisha salamu za shirikisho hilo katika hafla za Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyo adhimishwa Kitaifa Mkoani Singida leo Aprili 28, 2025.