Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa (Mb.), ametembelea banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) inayoshiriki katika Maonesho ya 73 ya Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege (ACI Africa), yanayofanyika katika viwanja vya Mount Meru Hotel, Arusha. Maonesho haya yanafanyika sambamba na Mkutano wa 73 wa Baraza hilo kwa Kanda ya Afrika.
Mheshiwa Waziri Mkuu ameridhishwa na jitihada za kukuza sekta ya Usafiri wa anga nchini.
Awali Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Bw. Salim Msangi, ambaye alimueleza kwa kina juhudi mbalimbali zinazotekelezwa na Mamlaka katika kuboresha miundombinu ya Usafiri wa Anga, kuimarisha usalama wa safari za anga, pamoja na kutumia teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma.
Maonesho haya yamekusanya pamoja wadau wa sekta ya viwanja vya ndege kutoka ndani na nje ya Afrika, yakilenga kubadilishana uzoefu, kuonesha mafanikio ya sekta ya usafiri wa anga, na kujadili mikakati ya maendeleo endelevu katika sekta hiyo muhimu.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Salim Msangi wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 73 wa Baraza la Kimataifa la Viwanja vya Ndege (ACI Africa) unaofanyika jijini Arusha.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisoma kipeperushi cha Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) alipotembelea na kupata maelezo mbalimbali kuhusu chuo hicho na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Salim Msangi.