Na Belinda Joseph-Songea DC.
Halmashauri ya Wilaya ya Songea imejipanga kwa mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, unaotarajiwa kuingia Mei 10 kupitia Kata ya Mpandangindo na kufanya mkesha katika Kata ya Magagura, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea mafanikio ya maendeleo katika maeneo yote ya Halmashauri hiyo.
Akizungumza katika Mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani wa robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2024/2025, uliofanyika Aprili 29, 2025 katika Ukumbi wa Halmashauri Lundusi, Mkurugenzi Mtendaji Bi. Elizabeth Mathias Gumbo amewataka viongozi na wananchi kushiriki kwa wingi kwenye shughuli hiyo muhimu ya kitaifa.
“Tunatarajia kupokea Mwenge wa Uhuru na tunawaomba viongozi wote, wananchi na wadau wa maendeleo kushiriki kikamilifu, Tukio hili si la kawaida ni nafasi ya kuonesha na kusherehekea mafanikio yetu kama Halmashauri,” alisema Bi. Gumbo.
Katika mkutano huo, Baraza la Madiwani likiongozwa na Makamu Mwenyekiti Simon Kapinga, limeipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa kila kata ndani ya Halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Viongozi pia walimpongeza Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Peramiho kwa mchango wake mkubwa, hususan kwa kuhakikisha upatikanaji wa madaktari bingwa waliowahudumia wananchi wa Songea.
Mkutano huo umejadili ajenda 10 muhimu na uliambatana na uwasilishaji wa taarifa kutoka kwenye kamati mbalimbali za Halmashauri, ikiwemo Kamati ya Maadili, Elimu Afya na Maji, Uchumi Ujenzi na Mazingira, Kudhibiti UKIMWI, pamoja na Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango.