Katika kuadhimisha Maonesho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, ametembelea banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Akiwa banda la TCAA , Mheshimiwa Hemed alipata maelezo kuhusu huduma na majukumu ya TCAA pamoja na miradi inayoitekeleza kutoka kwa Meneja wa Kituo cha TCAA katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume(AAKIA), Bw. Mohamed Ali Mohamed.
Katika maelezo yake, Bw. Mohamed pia alimueleza Mheshiwa Hemed namna TCAA inavyosimamia usalama wa safari za anga, kuratibu huduma za Uongozaji ndege, pamoja na kuendeleza teknolojia za kisasa kuhakikisha kunakuwa na ufanisi na maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini na visiwa vya Zanzibar kwa ujumla.
Mheshimiwa Hemed alipongeza jitihada za TCAA katika kuimarisha huduma za usafiri wa anga na kuhimiza mamlaka hiyo kuendelea kuboresha huduma kwa maslahi ya taifa na wananchi.
Maonesho hayo ya Mei Mosi yanazileta pamoja taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi kuonesha huduma na mafanikio yao katika kuunga mkono maendeleo ya kitaifa.
