Mbunge wa Jimbo la Madaba na Mwenyekiti wa Katai ya kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala Joseph Kizito Mhagama, amesema Kampeni ya Mama Samia Legal Aid imekuwa suluhisho la muda mrefu kwa wananchi waliokuwa wakikosa huduma za kisheria kwa sababu ya umbali pamoja na gharama.
Akizungumza Bungeni Aprili 30 wakati wa kujadili mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria, Mhagama amesema kampeni hiyo imeanza kufungua milango ya haki kwa Watanzania wengi, hasa waishio vijijini ambako huduma hizo zilikuwa adimu.
“Hii si tu kampeni ya kisheria, bali ni harakati ya kijamii inayowawezesha wananchi kuunganika moja kwa moja na mfumo wa haki,” alisema Mhagama. “Ni hatua ya kujenga taifa lenye misingi imara ya amani na utulivu wa kweli.”
Mbunge huyo amesema kwa kupeleka huduma hizo karibu na wananchi, serikali imeondoa vikwazo vilivyokuwa vikiwanyima watu haki zao kwa muda mrefu, Ameongeza kuwa kampeni hiyo inaashiria utekelezaji wa vitendo wa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kusogeza huduma kwa wananchi wote bila ubaguzi.
Mhagama pia amelitaka Bunge kutambua na kuunga mkono juhudi za viongozi wa sekta ya sheria, akiwataja Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro; Naibu Waziri Jumanne Sagini; Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari; na Katibu Mkuu Eliakimu Maswi, kwa kuhakikisha utekelezaji wa kampeni hiyo unaendelea kwa mafanikio.
Kwa maoni yake, mafanikio ya Mama Samia Legal Aid ni kielelezo cha ushirikiano wenye tija kati ya serikali na wananchi, ambao unalenga kujenga mfumo wa haki unaoaminika, unaofikika, na unaowajibika kwa wote.