Katikati ni Mratibu wa bonanza la Mac D linalofanyika kwa msimu wa pili Denzel Deogratius Rweyunga, Kushoto Afisa Masoko Muandamizi Albert Mboto na Meneja Msaidizi wa Zak’s Bay Liquar Store Valeria Msaki.
Na Khadija Kalili
UONGOZI wa Mac D Wine & Spirits umetangaza tarehe ya kufanyika bonanza lake katika awamu ya pili ambapo litaanza asubuhi saa 12:00 kutakuwa na mbio za kujifurahisha ‘Fun Run’ zitakazojulikana kwa jina la ‘Mac D Fun Run 2025’ .
Akizungumza na Waandishi wa Hbari leo tarehe 01 Mei 2025 kwenye Ukumbiwa EB Twenty Five uliopo Mbezi Makonde Jijini Dar es Salaam Mratibu wa bonanza hilo Denzel Deogratius Rweyunga amesema kuwa bonanza hilo linalofanyika kwa msimu wa pili litafanyika tarehe 07 Juni 2025 ambapo pia mbio hizo zitaanza katika Viwanja vya Chuo Cha Taifa Cha Jeshi (National Defence CollageNDC) Kunduchi Jijini Dar es Salaam.
“Washiriki wa mbio za KM 10 na KM5 wataanza mbio majira ya saa moja asubuhi kutoka Chuo Cha NDC wataelekea uelekeo wa kwenda Ununio na watakapofika katika Uwanja wa mpira unaofahamika kama Ununio Playground karibu na Kanisa la Roman Catholic watageuza hapo na kurejea katika uwanmja wa NDC.
Amesema kuwa lengo kuu la mbio hizi kwa mwaka huu ni kuunganisha jamii katika kuboresha afya na na kuwa wakakamavu katika kufanya mazoezi na kulenga kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza kufahamiana na kutengeneza marafiki wapya.
“Tunawaalika watu wote mtu mmoja mmoja, vikundi vya wakimbiaji na taasisi mbalimbali kushiriki pamoja nasi na baada ya kujisajili mshiriki atapata Tshirt bure na kwa yeyote anayependa kushiriki ajisajili kupitia www.macdbonanza .co.tz, vituo vingine vya usajili ni pamoja na EB Twenty Five Mbezi Makonde, Mac D Wines & Spirits Kunduchi, Zaks Bay Boko Magengeni na Leather Men Mabatini Kijitonyama Dar es Salaam.
“Msimu wa pili wa bonanza letu tutaanza na Fun Run hizi ni mbio za kujifurahisha na kuweka miili yetu katika hali nzuri ya kiafya ambapo hakuna mshindi wala zawadi yeyote itakayoshindaniwa bali washiriki wote watapatiwa fulana na namba ya kukimbia bure pia Kituo cha ITV kitarusha matangazo hayo mubashara” amesema Rweyunga.
Mratibu huyo ameongeza kwa kusema kuwa baada ya Fun Run kumalizika jioni kuanzia saa 10 timu mbili ambazo ni Mac D FC na IPP Media watashuka dimbani na katika mchuano wa mwaka huu mshindi ataondoka na Kombe na mechi hii itatangazwa mubashara na kituo cha Radio One.
Wakati huohuo Rweyunga ametoa shukrani kwa wadhamini wa bonanza hilo sambamba na kuwatambulisha katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam.
“Bonanza la mwaka huu limeandaliwa katika viwango vya juu , tunawashukuru sana wadhamini wetu ambao wamejitokeza kutuunga mkono ambao ni ITL, Bonite Bottlers (Kilimanjaro Drinking Water),Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Isumba Trans Limited , Zaks Bay Liquar na Pwani Inland Clearance and Depot (PICD).