Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila ameongoza maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani Mei Mosi Mkoani humo na kuwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa umahiri na uadilifu huku wakiamini kuwa Serikali inawapenda na inaendelea kushughulikia changamoto zao
RC Chalamila akizungumza Jijini Dar es salaam leo katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Mei Mosi yaliyofanyika kimkoa kwenye viwanja vya Tanganyika Perkas, amewataka wafanyakazi kufanyakazi kwa uadilifu bila kufanya ubadhilifu kwenye utendaji wao ili kila mwananchi anufaike na utumishi wao kwani Serilali inaendelea kushughulikia changamoto zao
Aidha RC Chalamila ameeleza kusikitishwa na baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu wanaopelekea baadhi ya wananchi kuichukia Serikali kutokana kutowatendea haki pale wanapohitaji huduma mbalimbali ambapo amesema kutowavumilia watumishi wa aina hiyo endapo tabia hizo zitajitokeza hatua za kisheria zitachukuliwa,ametolea mfano watumishi waliovamia saluni ya mmoja wa wakazi wa Mkoa huo na kumuambia anakosa la kutoa huduma bila kukamilisha taratibu za kupima afya kwa wahudumu hivyo waliwataka kulipa shilingi laki sita ambapo amesema huo sio utumishi bora wa umma.
Vilevile RC Chalamila ametumia maadhimisho hayo kuwataka wafanyakazi Mkoani humo kushiriki uchaguzi mkuu ili kupata viongozi bora watakaosaidia kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuleta maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule akizungumza kwa niaba ya wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Dar es salaam amesema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dkt Samia ameendelea kuifungua nchi kiuchumi hivyo amewataka wafanyakazi kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais kwa kuendelea kufanya kazi vyema huku akiwataka pia kushiriki uchaguzi
Akisoma risala kwa niaba ya wafanyakazi Mkoa wa Dar es salaam Katibu wa Chama cha mawasiliano na Uchukuzi Tanzania COTWUT Meshack Sarota amesema wanaamini Serikali sikivu ya awamu ya sita itaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kuongeza mishahara ikiwemo kwenye sekta binafsi,kupunguza kodi,kupunguza gharama za vifurushi kwenye bima ya afya na kuhakikisha wafanyakazi wote wanapata huduma bora za afya kupitia bima.
Sanjari na hayo ameomba Serikali kuimarisha usalama na Afya mahali pa kazi na kuondosha mikataba ya kazi ambayo ni kandamizi kwa wafanyakazi
Kupitia maadhimisho hayo wafanyakazi waliofanya vizuri kwenye utumishi wao wa mwaka mzima wamepatiwa zawadi ya fedha taslimu ambapo baada ya kupatiwa zawadi wafanyakazi hao wameeleza furaha yao kwa Serikali
Mwisho maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu isemayo “Uchaguzi mkuu 2025 utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya wafanyakazi sote tushiriki”.