Dar es Salaam, Aprili 25, 2025 – Ikiadhimisha miaka 10 ya
utoaji wa kadi za mikopo (credit card) nchini Tanzania, Absa Bank Tanzania
imezindua Absa Infinite Card, kadi ya kifahari inayolenga kuwahudumia wateja wa
hadhi ya juu kwa huduma za kifedha zilizoboreshwa na uzoefu wa kipekee wa
maisha.
Katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Aprili 25, 2025 jijini
Dar es Salaam, wadau wa sekta ya fedha, wateja muhimu na viongozi wa taasisi
walishuhudia tukio hilo la kihistoria.
Mgeni rasmi alikuwa Bi. Lucy Charles-Shaidi, Mkurugenzi wa
Mifumo ya Malipo ya Kitaifa kutoka Benki Kuu ya Tanzania, aliyemwakilisha
Gavana wa benki hiyo.
Absa Infinite Card inapatikana kwa njia ya kadi ya kawaida
ya benki (debit) na kadi ya mkopo (credit), na inatolewa kwa pesa ya Shilingi
za Tanzania pamoja na Dola za Marekani.
Kadi hii imebuniwa kukidhi mahitaji ya wateja wanaotafuta
ubora, usalama na upatikanaji wa huduma duniani kote.
Miongoni mwa faida zake ni bima ya safari za kimataifa,
kupata huduma za chakula, vinywaji na mapumziko katika viwanja vya ndege zaidi
ya 1,200, bei ya punguzo katika manunuzi, bima ya kufuta tiketi za safari, na
udhamini wa bidhaa za muda mrefu.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Absa
Bank Tanzania, Bw. Obedi Laiser, alisema kadi hiyo inaakisi mahitaji ya
Watanzania wanaotamani huduma bora za kifahari za benki.
“Absa Infinite Card si tu kifaa cha malipo, bali ni tiketi
ya kuingia katika maisha ya ubora wa hali ya juu. Tunataka wateja wetu
wafurahie urahisi, usalama na hadhi inayotokana na kutumia kadi hii mahali
popote duniani,” alisema Bw. Laiser.
Aliongeza kuwa kupitia uzinduzi huu, Absa inalenga pia kuchochea
matumizi ya kadi za mikopo nchini, akibainisha kuwa kiwango cha matumizi ya
bidhaa hizo bado kiko chini.
“Tunafanya uwekezaji mkubwa katika elimu kwa wateja ili
kuhakikisha Watanzania wanaelewa thamani ya usalama, urahisi na faida
zinazotolewa na kadi za mikopo,” alisema.
Kwa upande wake, Bi. Charles-Shaidi kutoka BoT aliipongeza
benki hiyo kwa kuendeleza juhudi za ubunifu, akibainisha kuwa bado kuna fursa
kubwa ya kuendeleza matumizi ya bidhaa za kadi za mikopo nchini.
“Bidhaa za kadi ya mikopo bado ni ngeni kwa Watanzania
wengi. Tunazihimiza benki kuwekeza zaidi katika ubunifu na elimu kwa wateja ili
kuchochea matumizi sahihi,” alisema.
Alisema Benki Kuu itaendelea kushirikiana na sekta binafsi
kuendeleza ujumuishaji wa kifedha na matumizi ya teknolojia za kisasa za
malipo.
Uzinduzi wa Absa Infinite Card ni matokeo ya msingi wa
mafanikio ya benki ya Absa tangu mwaka 2015, ilipoanzisha kadi ya kwanza ya
mikopo, ikishirikiana na mtandao wa Visa.
Mkurugenzi wa Huduma za Wateja wa Rejareja wa Absa, Bi. Ndabu
Swere, alisema nguvu ya benki hiyo haiko tu kwenye bidhaa, bali pia kwenye watu
wanaotoa huduma hizo.
“Kwa kadi ya Infinite, wateja wetu hawapati tu kadi, bali
wanapata uzoefu wa huduma binafsi, unaoendeshwa na timu iliyojitolea
kuwahudumia kwa viwango vya kimataifa,” alisema.
Kwa hatua hii, Benki ya Absa Tanzania inaendelea kusisitiza
dhamira yake ya “Kuiwezesha Afrika ya kesho, stori moja baada ya nyingine,”
ikilenga kuimarisha ushirikishwaji wa kifedha na kuchochea maendeleo ya sekta
ya kibenki kwa ubunifu na huduma bora.