Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya kudumu ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wamezipongeza Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar kwa kuendelea kuboresha maisha ya wananchi wa pande zote mbili kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Wajumbe wa kamati hiyo wamesema kwa upande wa Zanzibar kaya masikini 53000 zimefikiwa na TASAF na maisha yao yamekuwa bora kwani wengi wao wamepiga hatua ya kimaendeleo ikilinganishwa na awali kabla ya kuwa katika mradi huo.Pia Mfuko huo umeboresha miundombinu mbalimbali kwa kutumia walengwa wa Mfuko huo.
Akizungumza leo Mei 2,2025 baada ya kufanya ziara katika ofisi za TASAF jijini Dar es Salaam na kupokea taarifa ya utekeleza wa mradi wa mfuko huo kwa upande wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Mwanaasha Hamis Juma amesema wanatoa shukrani kwa Serikali zote mbili kwa kuamua kusaidia kaya masikini kupitia Mfuko huo.
“Tupo katika ziara zetu za kazi za kawaida na tunaelekea katika Bunge la Bajeti , hivyo tumekuja kwa wenzetu kuona na kupata taarifa kuhusu TASAF na moja katika hizo taarifa za Mfuko huu imesaidia kaya masikini na kuboresha miundombinu lakini kuwezesha kaya masikini katika mradi huu wameweza kunufuka na ni Tanzania kwa ujumla ikiwemo Zanzibar.
“Kamati ya Bajeti imekuwa ikiona maendeleo na taatifa mbalimbali kuhusu TASAF kwa hiyo leo temukuja kuona mafanikio na changamoto lakini mengi mafanikio kwa maana wale walengwa kaya masikini wamefikiwa na mradi huu na wameweza kujinasua kiuchumi.
“Katika zile changamoto na mradi mnapoelekea kumalizika tulikuwa tunaiomba Serikali na kuishauri kupata namna nyinyine bora ili mradi uendelee uweze kufikia wengine zaidi na zaidi.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shedrack Mziray amesema wamepata bahati ya kutembelewa na Kamati ya Kudumu ya Bajeti Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambapo amefafanua kuwa mradi wa TASAF unatelelezwa katika pande zote mbili kwa maana ya Zanzibar na Bara.
Amefafanua kwa upande wa Zanzibar mradi unaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Seeikali ya Mapinduzi Zanzibar na kwamba wiki ijayo wanaanza vikao vya bajeti hivyo wameona ni vizuri katika maeneo wanayoyasimamia waangalie utekelezaji na kupata taarifa fupi.
“Tumewaeleaa maendeleo ya mradi na Kwa upande wa Zanzibar tunashugulika na walengwa 53000 na ujumbe mkubwa ambao tumeipeleka mradi huu umekuwa ukitekelezwa kwa kuanzia mwaka 2021 kipindi hiki Cha pili na kinakwenda kukamilika Septemba mwaka huu.
“Kwahiyo kwa sasa tunawaelewesha wananchi kuhusu ruzuku ambazo tunawapatia kila mwezi pamoja na shughuli nyingi ambazo wamekuwa wakizifanya walengwa ruzuku zitasistishwa kwa muda kuanzia Septamba mwakani.Ujumbe mkubwa Serikali iko katika maandalizi ya programu mpya ambayo tunategemea itaanza baada ya programu hii kukamilika.”
Hivyo amewaomba wananchi wawe na matumaini kwa mradi utaendelea baada ya kukamilisha mchakato wa programu mpya na watakwenda kutambua ambao hawakufikiwa katika awamu ya sasa hivyo watakuwa na walengwa wapya na wataendelea na taratibu kama ambavyo mradi mpya utaandaliwa,
Ameongeza kwa ujumla Wajumbe wameishukuru na wamekiri kwamba programu hiyo imeleta mabadiliko makubwa kwa kaya masikini upande wa Zanzibar kwasababu kati ya 53000 zaidi ya kaya 9400 zilifanyiwa tathimini na kuonekana zimeboreka kimaisha hali zao kiuchumi zimekuwa nafuu ,hivyo walikoma kupata ruzuku Julai mwaka 2024.
“Kwahiyo wameridhishwa na utekelezaji na wameipongeza TASAF kwa kazi nzuri wanaiyofanya kwa upande wa Zanzibar na wako tayari kuishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili nayo iweze kusimamia vizuri mradi na kuongeza bajeti katika mradi huu kwa kipindi kipya kinachokuja,”amesema Mziray.
Wakati huo huo Mjumbe wa Kamati hiyo Profesa Omari Fakih Hamad amesema wamekuja kujifunza na kuona utekelezaji wa shughuli mbalimbali za TASAF na wamejifunza kwamba changamoto ambazo zimekuwa zikilalamikiwa mpango kwa awamu zilizopita mpya unaokuja na kuendelea Serikali imekusudia kuboresha ili mpango uwe na ufanisi zaidi.
Ametoa mfano katika muongozo mpya sasa viongozi wa ngazi za chini ambao sio wa kuteuliwa na hawana mishahara kuingiza katika mpango wa TASAF wakati awali haikuwepo.
Pia amesisitiza kwamba kilichomfurahisha ni TASAF kushirikiana na bodi za elimu ya juu Zanzibar na Tanzania kuhakikisha vijana na wanafunzi kutoka kaya masikini hawapati shida katika mpango wa malipo.