Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe.Magdalena K.Rwebangira ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Mbeya kujitokea na kufika kwenye vituo vya kujiandikisha ili kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Pamoja na kuhakiki taarifa zao kwenye Daftari la Awali la Wapiga Kura ambalo limebandikwa katika kila kituo.
Mhe. Rwebangira ametoa wito huo leo Mei 03, 2025, ikiwa ni siku ya tatu toka kuanza kwa zoezi hilo baada ya kutembelea na kukagua vituo vya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Gana, Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Ilomba, Ofisi ya Mtendaji Kata ya Itezi na Ofisi ya Kata ya Igawilo vyote vikiwa ndani ya Jiji la Mbeya.
Zoezi hilo la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili limeanza Mei 01, 2025 na linatarajiwa kukamilika Mei 07, 2025, ambapo linafanyika sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura katika mikoa ya Geita, Mara, Kagera, Shinyanga, Mwanza, Tabora, Katavi, Simiyu, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa.