*Ni msomi wa elimu ya juu aliyoipata Canada na sasa ameamua kupiga Kambi Ruvuma
*Mkakati wake ni kuchangia maendeleo ya Jamii, kukuza thamani ya CCM
Na Belinda Joseph-Songea.
KATIKA kizazi cha sasa kinachotawaliwa na ndoto nyingi lakini vitendo vichache, jina la Amandius Jordan Tembo maarufu kama Toronto, linaibuka kama nembo ya matumaini mapya ya maendeleo katika siasa za Tanzania.
Ni kijana mwenye maono makubwa, ambaye licha ya kuishi na kusomea nchini Canada, hajawahi kuisahau ardhi ya nyumbani yaani Songea Mkoani Ruvuma.
Toronto ambaye kwa sasa na umri wa miaka 35 ni mzaliwa wa Mkoa wa Ruvuma akiwa na elimu ya juu kutoka Chuo Kikuu cha Toronto nchini Canada, aliyeamua kurejea nyumbani sio kwa ajili ya maisha yake binafsi, bali kwa lengo la kuchangia maendeleo ya jamii na kukuza thamani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), chama anachokiamini na kukipenda kwa dhati.
Kijana huyu amejiwekea malengo mahsusi ya kuhakikisha kila kata ndani ya Manispaa ya Songea inakuwa na ofisi ya kisasa ya CCM, anaamini chama kikubwa kama CCM kinahitaji miundombinu bora inayolingana na hadhi yake, na si vyema kuendesha shughuli za chama kwenye mazingira yasiyovutia au yaliyochakaa.
Kwa kutumia fedha zake binafsi, Toronto tayari amefanikisha ujenzi wa ofisi mbili za CCM. Ofisi ya kwanza ipo Kata ya Subira, na ya pili katika Kata ya Bombambili, ambayo imekamilika kwa asilimia 100 na kukabidhiwa rasmi kwa uongozi wa chama.
Ujenzi huo wa ofisi ya CCM Bombambili ambao umegharimu zaidi ya Sh.milioni 30 umefanyika ndani ya miezi mitatu tu, jambo lililopokelewa kwa pongezi kubwa kutoka kwa wanachama na wananchi.
Hafla ya kukabidhi ofisi ya Bombambili ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, ambaye alisifu juhudi za Toronto na kueleza ni mfano wa kuigwa na vijana wengine kwani ameonesha siasa ya kweli ni ile inayogusa maisha ya watu kwa vitendo, si kwa kauli peke yake.
Kwa Toronto, kujenga chama ni sawa na kujenga jamii, anasisitiza kuwa maendeleo hayaji kwa kusubiri serikali pekee, bali kila mmoja ana jukumu la kuchangia kadri ya uwezo wake, Ndiyo maana ameamua kuwekeza kwenye miundombinu ya chama, kwani anaamini ndipo msingi wa uongozi bora na maendeleo unapoanzia.
Anatumia msemo wa “Charity begins at home” kama dira ya maisha yake, Kwa hiyo kabla hajafikiria kuchangia maeneo mengine, ameweka mkazo katika kujenga Songea nyumbani kwao, na maono yake ni kuona Songea inakuwa jimbo la mfano, ambalo watu kutoka mikoa mingine wanakuja kujifunza kupitia mafanikio yaliyopatikana kwa mshikamano wa jamii.
Mbali na siasa, Toronto pia anajihusisha na miradi mbalimbali ya kijamii kama vile elimu, na uwezeshaji wa watoto Anaamini sio siasa pekee bali ni muhimu kuwa na moyo wa kujitolea katika namna mtu anavyogusa maisha ya watu huongeza mshikamano katika jamii.
Kwa kufanya haya yote bila kusubiri uteuzi wala cheo, Toronto ameweka wazi kuwa si lazima kuwa mbunge, diwani au kiongozi mkubwa ili uweze kuleta mabadiliko, Kinachohitajika ni dhamira ya kweli, moyo wa kujitolea na uzalendo wa dhati kwa taifa.
Anawapongeza viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya taifa hadi kata kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kujenga chama na taifa, Anampongeza Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, kwa uongozi wake wa mfano unaoweka mazingira rafiki kwa vijana kushiriki katika maendeleo ya nchi.
Toronto anaamini chama ni chombo muhimu katika maendeleo ya jamii na si tu jukwaa la kisiasa, Ndiyo maana anataka kuona CCM inakuwa karibu zaidi na wananchi kupitia uwepo wa ofisi bora katika kila kata, ambapo wananchi watapata huduma, ushauri, na kushiriki katika mchakato wa maendeleo.
Katika mahojiano mbalimbali, Toronto ameeleza lengo lake ni kuona CCM inaendelea kuwa chama madhubuti kwa vitendo na si kwa historia tu, anaamini kuwa historia nzuri ya chama inapaswa kuendelezwa na vijana wa kizazi hiki kwa kuonyesha matendo halisi.
Kwa maono na kasi aliyonayo, Toronto ameanza kujenga msingi wa siasa ya matendo inayotazama maslahi ya watu kwanza, Hii ni aina ya siasa inayowavutia vijana wengi wanaotaka kuleta tofauti bila ya kuwa na migongano au tamaa za madaraka.
Kwa sasa Toronto anajiandaa kuanza ujenzi wa ofisi nyingine kadhaa ndani ya Manispaa ya Songea, hatua inayothibitisha kuwa haishi kwa maneno bali anatimiza ahadi zake.
Anasema maendeleo ni mchakato unaohitaji mshikamano ambao unapaswa kuanzia kwenye familia, jamii, chama hadi taifa zima, Kwa Toronto maendeleo hayawezekani bila kujitolea, na ndio msingi wa mafanikio yake.
Hatua zake zimekuwa zikileta hamasa mpya ndani ya CCM, hususan kwa vijana, ambao sasa wanamtazama kama mfano wa kuigwa kwa siasa ya kizalendo na maendeleo.
Kupitia jitihada hizi, Toronto anaandika historia mpya ya ushiriki wa vijana katika siasa ya vitendo, siasa inayotanguliza jamii kabla ya maslahi binafsi.
Huyo ni Toronto kijana wa kizazi kipya anayewasha moto wa maendeleo kupitia chama chake, akijenga ofisi, akijenga jamii, na zaidi ya yote akijenga taifa.