Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga amesisitiza ushirikiano katika suala usalama hasa kwa wakazi wa maeneo ya mgodini.
Hayo amezungumza Mei 07, 2025 alipotembelea mgodi wa dhahabu wa ANGLO DE BEERS (T) LIMITED uliopo Kijiji cha Patamela Mkoani Songwe kwa lengo la kutathimini hali ya usalama na ustawi wa wachimbaji wa eneo hilo.
Kamanda Senga alipata wasaa wa kukutana na baadhi ya wafanyakazi pamoja na viongozi waandamizi wa mgodi huo wanaozunguka eneo hilo, ambapo alipongeza hatua zinazochukuliwa katika kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na wachimbaji hao na kueleza kuridhishwa na usalama wa mgodi huo na kuwataka kutambua kuwa hakuna kazi muhimu katika eneo la mgodi bila kuangalia usalama wa kazi.
“Nyinyi viongozi wa mgodi mnapaswa kuendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe ili kuimarisha hali ya usalama mgodini na kuepusha changamoto zinazoweza kuhatarisha ustawi wa sekta ya madini katika Mkoa huo” alisema Kamanda Senga.
Alisisitiza na kuwahimiza kuzingatia sheria na kanuni za uchimbaji madini ili kuhakikisha shughuli hiyo inakuwa endelevu na yenye manufaa kwa jamii inayowazunguka na taifa kwa ujumla.
Kwa niaba ya Viongozi wa mgodi huo Yasin Rashid ambaye ni Meneja Mkuu wa Mgodi huo alilipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe akieleza kuwa ushirikiano kati ya wachimbaji na vyombo vya usalama ni muhimu katika kuimarisha mazingira bora ya kazi na kulinda rasilimali za mgodi kwa maendeleo ya ukuaji wa uchumi wa nchi.