Na Mwandishi Wetu
JAJI Mfawidhi wa Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Salma Maghimbi Juni 17 mwaka huu anatarajia kusikiliza maombi ya kuongeza muda wa kukata rufaa dhidi ya mfanyakazi wa benki Ibrahim Masahi, aliyeachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Awali, ilidaiwa kuwa Masahi Januari 11, 2023 akiwa eneo la Mbezi Msakuzi ndani ya Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam alituhumiwa alimpiga Deogratus Minja kwa nyundo na kumsababishia kupata madhara makubwa ya mwili mwake.
Mahakama ya Kinondoni, baada ya kusikiliza kesi hiyo ya tuhuma za kujeruhi ilimuachia huru Masahi (mjibu maombi) kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka lolote.
Upande wa mashtaka kutokana na hukumu hiyo iliwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi Amos Rweikiza kwamba mshtakiwa katika ushahidi wake hakueleza jinsi alivyomtambua usiku wa tukio hilo.
Hata hivyo, upande wa mashtaka umedai kwamba katika kesi hiyo uliweza kuthibitisha shtaka kwa sababu shahidi wao alieleza jinsi alivyomtambua mshtakiwa Masahi kwa kutokana na mwanga wa taa uliyokuwepo eneo hilo la tukio.
Mjibu wa maombi (Masahi) kupitia wakili wake wamewasilisha majibu ya maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na Jamhuri (kiapo kinzani).
Katika ushahidi wake, Minja alidai kuwa tarehe hiyo saa mbili na nusu usiku alikuwa akipita nje ya geti la jirani yake Masahi, alimkuta kijana wa jirani huyo, baada ya kumuona alizungumza kwa kilugha kwa sauti kubwa ambae yeye hakuielewa.
Amedai kuwa ghafla kijana alikwenda mbele yake akamzuia asipite, geti likafunguliwa akatoka Masahi akimuhoji kwamba, yeye ni kama nani na amekwenda kumshtaki Serikali za Mitaa, ambapo hakumjibu kitu, kijana wa mjibu maombi akampiga ngumi.
“Aliinua shati lake juu akatoa nyundo akanipiga nayo kichwani baada ya kupata maumivu makali nilianza kukimbia huku nikipiga kelele za kuomba msaada,” Amedai Minja.