Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Hawa Tundui (kushoto) akikabidhi zawadi ya kumbukumbu kwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) kwenye Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali
**********************
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb.), amekipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuwatengenezea mazingira wanafunzi wa chuo hicho yanayohamasisha ubunifu, kujifunza mbinu za Ujasiriamali, uwekezaji na Biashara wakati wakiendelea na masomo yao chuoni hapo na hivyo kuwaandaa vyema kujiajiri na kutatua changamoto ya ajira na kuwawezesha kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa
Mhe. Kigahe ameyasema hayo wakati akimuwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb.), katika maadhimisho ya siku ya Chuo Kikuu Mzumbe na kambi ya Ujasiriamali iliyofanyika Mei 8,2025 Kampasi Kuu Morogoro na kuwataka wanafunzi hao kuitumia fursa hiyo vizuri kwa kufanya bunifu zinazoendana na kukua kwa teknolojia zitakazowezesha kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii na kuiwezesha Tanzania ya viwanda inayojitegemea kwa maarifa na teknolojia.
“Nimefurahishwa sana na tukio hili kwani inaonesha namna Chuo kikuu Mzumbe kinavyotekeleza kwa vitendo agenda ya Serikali ya kutaka vijana kupatiwa elimu na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri, kwani tumeona hivi karibuni Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amezindua sera mpya ya elimu inayotaka
Vijana kupatiwa mafunzo ya amali, lakini pia hivi karibuni Mhe. Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa Watanzania kwenda kusoma VETA”.Alisema
Aidha Naibu Waziri aliongeza kuwa chuo Chuo Kikuu Mzumbe kimekuwa kikitambulika kwa umahiri katika kufundisha masomo ya utawala na Menejimenti lakini sasa kimechukua hatua madhubuti kwa kuibeba agenda ya kujenga ujuzi na kuwapa vijana fursa za ubunifu kwa vitendo na kuwaomba kuendeleza programu hiyo kwakuwa ni jukwaa muhimu sana katika kuvumbua vipaji vya ubunifu kwa manufaa ya taifa zima
Kwa upande wake Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia masuala ya ubunifu wa biashara, Dkt. Lorah Basolile Madete, alikipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuandaa tukio na kuongeza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inaonyesha namna ambavyo vijana wanatakiwa kuziendea ndoto zao bila kuangalia vikwazo na mipaka na kwamba kambi kama hizo ni jukwaa la kulea na kukuza Wajasiriamali wengi wa sasa na wa baadaye kutoka ndani ya jamii.
Awali Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Hawa Tundui ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri alisema kuwa kambi hiyo imekuwa sehemu ya utamaduni wa kila mwaka wa Chuo Kikuu Mzumbe ambapo lengo lake ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa ubunifu na kuwahamasisha kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayosaidia kuleta maendeleo katika jamii.
Katika tukio hilo, Naibu Waziri alipata fursa ya kutembelea mabanda ya wanataaluma, wajasiriamali, na wabunifu, pamoja na kushuhudia mashindano ya uwasilishaji wa wazo la kibiashara ambapo washiriki walieleza mawazo yao ya kibunifu na kushindanishwa ambapo bi.Edna Laizer mwanafunzi kutoka kitivo cha Sayansi na Teknolojia (FST) aliibuka mshindi wa kwanza kwa kubuni kifaa cha kuchuja maji kwa matumizi ya vijiji na mijini
Katika hatua nyingine Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi, alisisitiza dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe kuendelea kuwa jukwaa la kukuza vipaji, ubunifu na ujasiriamali wa vijana kwa maendeleo endelevu ya Taifa na
kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha Vijana wanapatiwa elimu na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) (kushoto) akisalimiana na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Hawa Tundui (kulia) alipowasili chuoni hapo kuhudhuria tukio la Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) (kushoto) akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe alipowasili chuoni hapo kuhudhuria tukio la Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) (kushoto) akikagua mabanda mbalimbali ya maonesho na kuelezewa huduma zinazotolewa kwenye Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali
Msaidizi Mahsusi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Aloyce Gervas akiongoza itifaki ya utambulisho kwa washiriki wa Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Hawa Tundui akizungumza na washiriki wa Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali

Meneja wa Kitengo cha Ujasiriamali, Ubunifu na Uhusiano wa Kitasnia Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Emmanuel Chao akizungumza na washiriki wa Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Bi. Elina Laizer akielezea kuhusu ubunifu wake kwa washiriki wa Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali
Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango anayeshughulikia Masuala ya Ubunifu na Biashara Dkt. Lorah Madete akizungumza na washiriki wa Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) (kulia) akikabidhi zawadi ya pesa kiasi cha shillingi milioni moja kwa Mshindi wa kwanza mwenye Ubunifu wa kifaa cha kuchuja maji kwa matumizi ya mjini na vijijini Bi. Elina Laizer (kushoto) kwenye Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) (kulia) akikabidhi zawadi ya pesa kiasi cha shillingi laki saba kwa Mshindi wa pili mwenye ubunifu wa mfumo unaoitwa mazingira app Bw. Joseph Joseph (kushoto) kwenye siku ya mzumbe na kambi ya ujasiriamali.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) (kulia) akikabidhi zawadi ya pesa kiasi cha shillingi laki tano kwa Mshindi wa tatu wa ubunifu unaohusu mfumo wa usafirishaji unaoitwa rush, Bw. Valentino Simbo (kushoto) kwenye Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali

Mtoa Mada ambaye pia ni Mhitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe Wakili Shedrack Mofulu akizungumza na kutoa hamasa kwa vijana wakati wa Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) akizungumza na washiriki wa Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango anayeshughulikia masuala ya Ubunifu na Biashara Dkt. Lorah Madete (wa kwanza kushoto) na baadhi ya viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe waliohudhuria Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb.) (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango anayeshughulikia masuala ya Ubunifu na Biashara Dkt. Lorah Madete (wa kwanza kushoto) na baadhi ya viongozi wa Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe waliohudhuria Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali