Farida Mangube, Morogoro
Katika kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wamezindua rasmi kampeni ya kitaifa ya “Soma na Mti, Ishi na Mti” katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, ambapo miti 100,000 inatarajiwa kupandwa katika shule za msingi na sekondari kama sehemu ya mkakati wa kuhamasisha elimu ya mazingira miongoni mwa wanafunzi.
Uzinduzi huo umefanyika katika Shule ya Msingi Sululu na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dustan Kyobya, ambaye amesisitiza umuhimu wa kuelimisha watoto kuhusu utunzaji wa mazingira tangu wakiwa wadogo.
“Mpango huu utakwenda sambamba na upandaji miti pembezoni mwa barabara kuu ya Kidatu–Mlimba. Hii si kampeni ya miti tu, ni kampeni ya maisha, kwa kuwa mazingira bora ni msingi wa maendeleo endelevu,” alisema DC Kyobya.
Aidha ameipongeza TFS kwa kutoa miche bure kwa wananchi na kuongoza juhudi za kurejesha uoto wa asili unaopotea kutokana na ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira, ambapo amesisitiza yeyote atakayehusika na uharibifu wa mazingira, ikiwemo kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi, hatavumiliwa.
Amesema Miti ni kichocheo kikubwa cha mvua, husaidia kuhifadhi unyevu ardhini, na huchangia katika kutunza vyanzo vya maji – jambo linalosaidia kilimo, uzalishaji wa umeme, na usalama wa chakula.
Kwa upande wake, Mhifadhi wa Wilaya ya Kilombero, Bi. Zalina Hassan, alisema TFS imekwisha toa miche 6,000 katika awamu ya kwanza ya kampeni hiyo, ambayo itapandwa katika shule na maeneo ya barabara ya Kidatu–Ifakara.
“Natoa wito kwa wananchi kufika katika ofisi za TFS kuchukua miche inayotolewa bure na kushiriki katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi,” aliongeza Bi. Zalina.
Bi. Zalina amesema kuwa miti ina mchango mkubwa katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kufyonza hewa ukaa (carbon dioxide) na kutoa oksijeni. “Tunapopanda miti tunapunguza kiwango cha gesi chafuzi hewani, tunasaidia anga letu na mustakabali wa vizazi vijavyo,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa kampeni ya “Soma na Mti Tanzania” alisema lengo ni kuwahimiza wanafunzi kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu kushiriki kikamilifu katika kupanda na kutunza miti katika maeneo yao ya jamii.
Kampeni hii inalenga kuibua kizazi chenye uelewa wa mazingira, kuhifadhi vyanzo vya maji, na kuongeza mvua kwa ajili ya shughuli za kilimo na uzalishaji wa umeme – hasa katika wilaya yenye ardhi oevu kama Kilombero.