![]() |
Baadhi ya viongozi wakizungumza kwenye mkutano na wadau wa elimu uliofanyika, shule ya msingi Migunga. |
![]() |
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Migunga, Bw. Mkude Chahe akisoma taarifa ya shule kwa wadau wa elimu walipotembelea shule hiyo. |
![]() |
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Kitaifa ya Maadhimisho ya Juma la Elimu (GAWE) 2025, Bw. Greyson Mgoi akizungumza kwenye moja ya mikutano ya washiriki wa Maadhimisho ya Juma la Elimu (GAWE) 2025. |
![]() |
Shule ya Msingi Migunga pichani. |
Na Mwandishi Wetu, Katavi
WANACHAMA wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), wamepongeza juhudi zinazofanywa na wazazi/walezi pamoja na Umoja wa Ushirikishaji walimu na Wazazi (UWAWA) kujenga maboma kwa ajili ya kutatua changamoto za upungufu wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi.
Pongezi hizo zimetolewa na wadau hao wa elimu kwenye ziara zinazofanywa kutembelea shule kadhaa ndani ya eneo hilo, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya shughuli za Juma la Elimu Kitaifa (GAWE) 2025, zinazofanyika ndani ya Halmashauri ya Mpimbwe, mkoani Katavi.
Akizungumza katika mikutano ya wazazi, walimu, viongozi wa vijiji na kata, Mratibu Taifa wa TEN/MET, Bi. Martha Makala alisema “..Tumeona wazazi wamejenga maboma kupitia umoja wao wa UWAWA kimsingi hili ni jambo jema sana katika kuhakikisha upatikanaji wa elimu iliyo bora na jumuishi kwa watoto wote, pia napenda kupongeza wazazi na viongozi katika kuunga mkono juhudi za Serikali kushiriki kwa utekelezaji sera ya elimu bila ada maana naona idadi kubwa ya uandikishaji wa watoto shuleni.
Kwa msingi huu nawapongeza wazazi/walezi na viongozi wa ngazi mbalimbali za Serikali kuanzia ngazi za vijiji, kata, tarafa, wilaya na hadi mkoa kwa kitendo cha kusimamia Sera ya elimu bila ada shuleni, kwani inachangia kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya kupata elimu bila kikwazo na pia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga shuleni.
Aidha akizungumzia ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na shule, alitolea mfano Shule ya Msingi Migunga ambapo ilianzishwa mwaka 2020 ikiwa na wanafunzi 1232 na walimu watano, lakini hadi sasa inawanafunzi 2362 na walimu 17 jambo ambalo linaonesha ongezeko la wanafunzi ni eneo hili ni kubwa.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Migunga, Bw. Mkude Chahe alisema idadi kubwa ya wanafunzi shuleni hapo imekuwa changamoto ya ufundishaji kwa walimu kwani vyumba vya madarasa ni vichache ukilinganisha na mahitaji.