MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka wawekezaji, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali za Kimataifa kuja kuwekeza nchini pamoja na kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali hususani katika teknolojia.
Ameyasema hayo Mei 09, 2025 jijini Dar es Salaam katika kilele cha Kongamano la e-Learning Africa, ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali wa elimu.
Aidha Mhe. Abdulla amesema Tanzania imedhamiria kufanya mapinduzi makubwa ya maendeleo katika sekta elimu, teknolojia na uvumbuzi, hatua ambayo inalenga kuvutia Wawekezaji ndani na nje ya nchi.Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Kongamano la e-Learning Africa litachagiza maendeleo katika sekta mbalimbali barani Afrika ikiwemo elimu.
Amesema kuwa Kongamano hilo limetoa mwongozo wa namna gani elimu barani Afrika inapaswa kuwasilishwa kwa kutumia nyenzo mbalimbali za kidigitali.
“Kongamano la e-Learning Africa litachangia maendeleo ya sekta mbalimbali barani Afrika, hususan elimu, na kuiwezesha Tanzania kupiga hatua katika matumizi ya teknolojia na sayansi. Ameeleza kuwa kongamano hilo limetoa mwongozo muhimu wa kuwasilisha elimu kwa njia za kisasa za kidijitali”. Amesema Prof. Mkenda.
Nae Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry Silaa amesema kuwa serikali inatekeleza Mpango wa Miaka 10 wa uchumi wa kidijiti uliozinduliwa na Rais Samia Julai 2024, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya 2016.
Amesema miongoni mwa nyenzo muhimu za utekelezaji wa mpango huo ni ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA, ikiwemo kusambaza mtandao wa intaneti na ujenzi wa minara 758 ya simu.
Aidha Waziri Silaa ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa maandalizi mazuri ya kongamano hilo, na kwamba litachangia maendeleo ya elimu na kuitangaza Tanzania kimataifa.