Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ya nchini Tanzania na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) ya nchini Kenya zimekutana kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa udhibiti wa shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.
Mamlaka hizo zimekutana Jijini Dar es Salaam Mei 12 na 13, 2025 na kuhusisha baadhi ya viongozi na wataalam kutoka pande zote.
Akifungua kikao cha kubadilishana uzoefu kati ya Taasisi hizo, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni alisema kuwa tukio hilo ni muhimu kwa ustawi wa tasnia ya petroli nchini Tanzania na Kenya na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
“Tukio hili litasaidia, pamoja na mambo mengine, kuboresha ufanisi wa taasisi zetu katika kudhibiti shughuli za mkondo wa juu wa petroli na kuimarisha ushiriano wa kikanda”, aliongeza Sangweni.
PURA na EPRA zimebadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali yakiwemo sheria na kanuni za petroli, usimamizi wa data za petroli na mikataba ya uzalishaji na ugawanaji mapato.
Maeneo mengine ni leseni za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, na ushiriki wa wananchi katika miradi ya mafuta na gesi asilia inayotekelezwa.
