Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano na Masoko ya Chama cha Wasambazaji wa Huduma katika Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA), Dkt. Sebastian Ndege, akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 14, 2025, jijini Dar es Salaam.
KUELEKEA Kongamano Maalum la Sekta ya Madini, Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano na Masoko ya Chama cha Wasambazaji wa Huduma katika Sekta ya Madini Tanzania (TAMISA), Dkt. Sebastian Ndege, ametoa wito kwa Watanzania wanaomiliki kampuni zenye uwezo wa kutoa huduma katika sekta ya madini kujiunga na TAMISA ili waweze kupata taarifa muhimu zitakazowawezesha kunufaika na fursa zilizopo katika sekta hiyo.
“Ili kampuni ifanikiwe, jambo la kwanza ni kuwa na taarifa sahihi. Taarifa ni nguvu inayokupa uwezo wa kufanikisha jambo kwa ufanisi,” Amesema Dkt. Ndege.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 14, 2025, jijini Dar es Salaam, Dkt. Ndege alitangaza kuwa Mei 16, 2025, kutazinduliwa Kamati Maalum ya Mawasiliano na Masoko itakayoshughulika na utoaji wa taarifa kupitia makongamano mbalimbali.
“Tunawakaribisha wajasiriamali wote kushiriki kwenye kongamano litakalofanyika katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, ambapo Watanzania wanaotoa huduma kwenye sekta ya madini wataunganishwa na wadau muhimu,” ameongeza.
Kongamano hilo litaambatana na majadiliano ya ana kwa ana kuhusu nafasi ya Watanzania katika utoaji huduma kwenye sekta ya madini. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, sambamba na watendaji waandamizi wa wizara hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMISA, Bw. Peter Kumalilwa, amesema kuwa lengo kuu la kuanzisha kamati hiyo ni kuwa na chombo maalum cha kuratibu mawasiliano na masoko kwa ajili ya Watanzania wanaofanya kazi migodini.
Ameeleza kuwa katika bajeti ya serikali, kiasi cha shilingi trilioni 3.1 hutengwa kila mwaka kwa ajili ya masoko na mawasiliano, fedha ambazo TAMISA inatamani ziwanufaishe zaidi wajasiriamali wa ndani.
“Tumeona watu kutoka nje wakifanya kazi ambazo Watanzania wanaweza kuzifanya. Kupitia TAMISA tutajenga uwezo kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini na kuanzisha viwanda hapa nchini ili kutoa huduma ndani ya mipaka yetu,” amesema Bw. Kumalilwa.
Aidha, TAMISA imetoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajumuisha kwenye makongamano mbalimbali ambayo yamefungua fursa lukuki kwa Watanzania. Pia wamempongeza Waziri wa Madini kwa juhudi zake za kuwaunganisha na kampuni mbalimbali pamoja na wizara, ili kuhakikisha kampuni za Kitanzania zinajengewa uwezo na kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
“Tunahitaji kuwa na chombo cha pamoja kitakachowafikishia Watanzania taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo. Kuna Watanzania wengi wenye uwezo wa kutoa huduma migodini lakini hukosa taarifa muhimu,” amesema Kumalilwa.
Amehitimisha kwa kusema kuwa wameamua kuungana ili kutoa taarifa sahihi kwenye mnyororo mzima wa sekta ya madini, ili ziwafikie walengwa wote nchini.