Namtumbo – Ruvuma
Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Namtumbo unaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji safi katika vijiji vya Msisima na Mnalawi, mradi unaotarajiwa kuhudumia wakazi 4,081 mara utakapokamilika, hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 60 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 13, 2025.
Akizungumza Mei 15, 2025 mbele ya kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Namtumbo, Mhandisi David Mkondya, alisema kuwa kazi zilizokamilika hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa chanzo cha maji, ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji, uchimbaji wa mitaro, ulazaji na ufukiaji wa mabomba yenye urefu wa mita 7,100.
Wananchi wa vijiji vya Msisima na Mnalawi wameeleza shukrani zao kwa serikali kwa kuwaletea mradi huo muhimu, ambao wanaamini utamaliza changamoto ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, hususan kipindi cha kiangazi, pamoja na kupunguza hatari ya magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyo safi.
Akiongea mara baada ya kukagua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ussi, alisema kuwa ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati, unaotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila kijiji na mtaa unapata huduma ya maji safi na salama.
Mradi huu ulianza kutekelezwa tarehe 17 Oktoba 2023 na umebeba matumaini makubwa kwa wananchi wa maeneo husika katika kuboresha maisha na afya zao kupitia upatikanaji wa maji safi kwa wote.