Na Janeth Raphael MichuziTv – Chamwino Dodoma
RAIS wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan ameboresha taarifa zake za mpiga kura katika Kijiji Chamwino Ikulu, huku akiwataka watanzania kuwa wazalendo kwa kuchangamkia haki yao ya msingi ya kujiandikisha.
Uboreshaji wa taarifa za mpiga kura awamu ya pili ulianza Mei 16,2025 ambapo jana Rais Samia alihakiki taarifa zake katika kitongoji cha Sokoine Kijiji cha Chamwino Ikulu.
Rais Samia alifika saa 8.20 mchana na moja kwa moja alielekea katika kituo cha kupiga kura ambapo alitumia dakika 10.
Mara baada ya kumaliza kujiandikisha,Rais Samia alipata nafasi ya kuzungumza na Wananchi waliojitokeza ambapo alidai ametumia nafasi yake ya kikatiba kujiandikisha katika kituo cha Chamwino Ikulu.
“Nimeona nijiunge nanyi kama mnavyojua mimi ni mkazi wa Chamwino huko nyuma nimepiga kura sehemu nyingi.Nimekuja kurekebisha taarifa zangu huko nyuma nilikuwa nikijiandikisha na kupiga kura Zanzibar mwaka huu inabidi nipige hapa Makao Makuu ya Nchi na Serikali,”alisema Rais Samia.
Aidha,Rais Samia amesisitizia wananchi kujitokeza kupiga kura kwani huo ni mzunguko wa pili na wasipofanya hivyo watakuwa wamepoteza haki yao ya msingi.
“Niwaombe tuje tupige kura huu ni mzunguko wa pili tukikosa huko mbele huwezi kurudia ili turudishe Serikali.Nitumie fursa hii kuwashukuru nawaomba waiteni ambao hawajaja waje,”alisema Rais Samia.
“Kazi inachangamoto wastahimili wale wanakuja kujiandikisha waendelee kadi zimepungua subiri.Nataka niwahakikishie kwa mipango mizuri kila mwenye haki ya kuandikishwa ataandikishwa,”alisema Rais Samia.
Rais Samia alisema : “Kutokujitokeza ni kukataa haki ya kikatiba suala unajiuliza ww ni mzalendo wa aina gani?
Nenda kapige kura wewe ukitaaa wenzako wataenda kumweka wanaomtaka suala kubwa hapa ni uzalendo hii ni fursa kubwa ni vyema kila mtanzania ajitokeze atumie nafasi hii,”alisema Rais Samia.
Kwa upande wake Afisa Mwandikishaji kutoka Majimbo ya Chamwino na Mvumi,Godfrey Mnyamale alisema wananchi wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha ambapo amedai malengo ni kuwaandikisha wananchi 280,000.
Alisema zoezi hilo ni Maalimu kwa wale ambao waliokosa nafasi ya kujiandikisha awamu ya kwanza,pamoja na wale ambao wanataka jkubotesha taarifa pamoja na wale waliokosa sifa.
“Kama alivyosema Mheshimiwa Rais,niwaombe wananchi wa Majimbo haya ya Chamwino na Mvumi kutumia fursa hii,”alisema Mnyamale.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akishiriki zoezi la uboreshaji wa taarifa zake katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura leo tarehe 17 Mei, 2025 katika Ofisi ya Serikali ya Kijiji, Chamwino mkoani Dodoma ambapo pia aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari hilo.