Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe.Peter Serukamba, ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo kuhakikisha wanadhibiti utoaji wa risiti feki kwa bidhaa mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki za kutoa risiti (EFD) ili kuongeza mapato ya serikali.
Akizungumza leo Mei 19, 2025 ofisini kwake baada ya kupokea ugeni wa timu ya maafisa kutoka TRA Makao Makuu uliofika kwa ajili ya kuanza kampeni ya utoaji elimu kwa mlipakodi kwa njia ya “Mlango kwa Mlango”, Serukamba alisema kuwa ni muhimu kwa maofisa wa TRA kutumia elimu na si nguvu wakati wa kukusanya kodi.
Aidha, Mhe Serukamba amewahimiza wafanyabiashara wote mkoani Iringa kupokea elimu hiyo kutoka kwa wataalamu wa TRA na si kufunga maduka au kuwaogopa.
Sambamba na hilo kampeni ya “Mlango kwa Mlango” inalenga kuelimisha wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, matumizi sahihi ya mashine za EFD, na kutoa risiti kwa kila mauzo.
”Ni muhimu kwa kila mfanyabiashara kutoa risiti halali kwa kila mauzo na kulipa kodi stahiki na hii itasaidia serikali kupata mapato ya kutekeleza miradi ya maendeleo,”amesema Serukamba
Peter Jackson ni Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, ameeleza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha ushirikiano kati ya TRA na wafanyabiashara.
Amesema, hatua hiyo inalenga kubadilisha mtazamo wa wafanyabiashara juu ya mamlaka hiyo na kuongeza uwazi katika ulipaji kodi.
Lengo letu si kuwatisha wafanyabiashara, bali kuwashirikisha na kuwasaidia kuelewa kwa nini ni muhimu kulipa kodi kwa hiari. Pia tunataka kila mfanyabiashara aichukulie TRA kama mshirika wa maendeleo na sio adui wa biashara zao,” amesisitiza.
Kwa upande wao Wafanyabiashara waliofikiwa na Elimu hiyo wameishukuru Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa uamuzi wa kutoa elimu ya mlipakodi mlango kwa mlango” maarufu kama door to door, wakisema kuwa hatua hiyo imewasaidia kupata uelewa mpana kuhusu masuala ya kodi na umuhimu wa kutumia mashine za kielektroniki za kutoa risiti (EFD).
Katika kampeni hiyo iliyoratibiwa kwa ushirikiano kati ya ofisi ya TRA makao makuu na ya mkoani Iringa, maafisa wa mamlaka hiyo walitembelea maduka ya wafanyabiashara na kutoa elimu ya moja kwa moja huku wakipokea maoni na changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara.
Kelly Mnyawami ni mmoja wa wafanyabiashara eneo la Kihesa Manispaa ya Iringa ambaye amesema, kutokana na elimu aliyoipata kupitia kampeni hiyo, hivi sasa atahakikisha analipa kodi kwa hiari tena kwa wakati.
Amesema kama kampeni hiyo itaweza kuwafikia wafanyabiashara wote nchini kutakuwa na ongezeko kubwa la makusanyo ya kodi ukilinganisha na ilivyo sasa.