GEITA MJINI: KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Amos Makalla amesema serikali imeazimia kuwainua wachimbaji wadogo wa madini lengo ni kuhakikisha uchumi wa wachimbaji wote unakuwa kwa pamoja.
Makalla ameeleza hayo leo Mei 20 wakati akizungimza na wananchi wa Geita Mjini mkoani Geita, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku saba katika mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Kagera, Geita, Mwanza Simiyu na Shinyanga.
Akifafanua hilo Makalla amesema azma ya serikali ikiongozwa na Rais Samia ni kuwajali wachimbaji wadogo wa madini na ndo maana rais wao na wachimbaji wameendekea kumuunga mkono na jitihada zake kwa sababu ameingia kwenye rekodi ya kuwajali wachimbaji wadogo.
Ameeleza hilo akisisitiza kuwa wachimbaji wakubwa waliopo alianza kama wachimbaji wadogo, hivyo wachimbaji hao wakipewa fursa wataweza kukua na kuajiri watu na kuongeza mapato na azma ya serikali ya CCM ni kuwajali wachimbaji wote kuhakikisha uchumi unakuwa kwa pamoja.
Makalla amewasisitiza wananchi kuwapuuza watu wanaowahadaa wananchi kwa kusema kuwa wachimbaji wadogo wamesahaulika, kwani kuwepo na madini katika eneo hilo kunaonyesha kuna mtu muadilifu anayesimamia rasilimali hizo.