Wakala wa Vipimo Tanzania wamepokea na kusimika mtambo mpya
wa kisasa wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 400, kwa ajili ya
kuhakikisha dira za maji. Mtambo huo una uwezo wa kupima hadi dira 1,000 kwa
siku, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na usahihi katika uhakiki wa mita za
maji nchini.
Kupitia maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani, Wakala wa
Vipimo wameendesha zoezi la kutoa elimu kwa wananchi pamoja na madereva wa
malori katika kituo chao kilichopo Misugusugu, Kibaha mkoani Pwani. Elimu hiyo
ililenga kuwaeleza wananchi umuhimu wa uhakiki wa dira za maji pamoja na faida
zake katika matumizi ya kila siku ya maji majumbani na kwenye taasisi
mbalimbali.
Akizungumza katika zoezi hilo, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi
wa Wakala wa Vipimo, Bw. Karim Mkorehe, alitoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwapatia mtambo
huo mpya wenye uwezo mkubwa wa kuhakiki dira za maji.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Vipimo katika
Kituo cha Misugusugu, Bw. Gaudence Gaspary, alisema kuwa elimu hiyo imetolewa
kwa makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo madereva wanaopata huduma katika
kituo hicho. Alifafanua kuwa dira ya maji inapaswa kuhakikiwa angalau mara moja
kwa mwaka ili kuhakikisha usahihi wa gharama za matumizi ya maji.
Aidha, baadhi ya wananchi waliopatiwa elimu hiyo walieleza
kufurahishwa na mafunzo hayo huku wakikiri kuwa wengi wao hawakuwa na uelewa
juu ya uwepo wa huduma za uhakiki wa mita za maji.