Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kushirikiana na Hospitali ya Misheni Ndanda inayomilikiwa na Shirika la Wabenedictine, wameanza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa Mitanga-Ukombozi ambao unatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 1,984 wa vijiji vya Mitanga na Ukombozi, Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara.
Mradi huo utagharimu jumla ya Shilingi 162,764,290 ambapo Hospitali ya Ndanda imechangia Shilingi 124,178,920 kwa ajili ya kufanya utafiti wa maji, uchimbaji wa kisima, ununuzi wa mitambo ya kusukuma maji, ujenzi wa mnara, uwekezaji wa tenki lenye ujazo wa lita 10,000 na ulazaji wa bomba lenye urefu wa mita 2,730.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Newala, Sadick Nsajigwa, alisema kuwa ofisi yake imetoa mabomba yenye urefu wa mita 2,730, tenki la kuhifadhi maji, jenereta moja, na kujenga uzio kuzunguka eneo la tenki, kazi iliyogharimu Shilingi 29,395,370.
Aidha, wananchi wa vijiji hivyo wametoa mchango wa Shilingi 9,190,000 kwa kutoa eneo la ujenzi bure, kuchimba na kufukia mitaro kwa ajili ya ulazaji wa mabomba.
Akizungumza kabla ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi, alisema kuwa mradi huo unaotekelezwa tangu Novemba 2024 na unatarajiwa kukamilika Juni 2025, tayari umefikia asilimia 75 ya utekelezaji.
Nsajigwa alieleza kuwa mradi huo umetekelezwa kwa shughuli mbalimbali muhimu ikiwemo utafiti wa upatikanaji wa maji chini ya ardhi, uchimbaji wa kisima, ununuzi wa mitambo, ujenzi wa mnara, uwekezaji wa tenki la maji, ulazaji wa mabomba pamoja na ujenzi wa uzio.
Kwa mujibu wake, mradi huo utasaidia kupunguza adha ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa vijiji hivyo ambao hapo awali walilazimika kutembea zaidi ya kilometa mbili kila siku kwenye mabonde na milimani kutafuta maji.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ismail Ali Ussi, aliwapongeza wataalamu wa RUWASA Wilaya ya Newala na Mkoa wa Mtwara kwa usimamizi bora wa miradi ya maji na kusisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa watumishi wa umma.
“Mradi wa maji Mitanga-Ukombozi umetekelezwa kwa viwango na kwa matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Serikali pamoja na wafadhili kupitia Hospitali ya Misheni Ndanda. Naomba wananchi walinde miundombinu ya mradi huu na kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuondoa kero ya maji,” alisema Ussi.
Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini, Maimuna Mtanda, alishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza mradi wa visima vitano katika jimbo lake chini ya mpango wa visima 900-5 kila jimbo, ambao amesema utapunguza kero ya muda mrefu ya maji kwa wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mitanga, Hassan Hamis, alisema kuwa tangu kijiji hicho kilipoanzishwa mwaka 1969, hakijawahi kupata huduma ya maji safi na salama, na mradi huu utaleta maendeleo kwa kuwa wananchi sasa wataweza kutumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi badala ya kutafuta maji.