Na WAF – Geneva, Uswisi
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutokomeza Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele (Neglected Tropical Diseases – NTDs) ikiwemo kufanya usambazaji wa dawa aina ya ‘Mectzan’ kwa wananchi walio kwenye hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa matende na mabusha pamoja na usubi kwa asilimia 100.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Mei 20, 2025 kwenye kikao cha pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 78 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaoendelea Geneva, Uswisi.
“Mafanikio mengine tuliyoyapata ni kupunguza asilimia ya watu waliokuwa na ugonjwa wa Usubi (river blindness) katika wilaya 27 za Tanzania kwa kiasi kikubwa kutoka asilimia 45-95% mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 0-3.5% katika kipindi cha miaka 20 iliyopita,” amesema Waziri Mhagama.
Amesema, Tanzania imeungana na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na wafadhili wengine wanaotoa dawa aina ‘Ivermectin’ katika kuadhimisha mafanikio makubwa yaliyofikiwa ya kutokomeza matende, mabusha pamoja na usubi kwa kufikia matibabu Billion Tano (5) na kuashiria kuendeleza juhudi hizo (5 billion treatment and counting).
Aidha, Waziri Mhagama amesema magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza athari za maendeleo ya kijamii na kiuchumi ambayo yanasababisha kuongezeka kwa umasikini.
“Ndio maana kama Tanzania tumeamua kwa dhati chini ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kupambana na magonjwa haya kwa kutoa kipaumbele endelevu katika kuyatokomeza ndani ya ajenda yetu ya afya ya kitaifa na mgawo wa rasilimali.
Waziri Mhagama amesema mafanikio hayo yamewezekana kupitia ushirikiano imara uliopo, hivyo ameomba kuendelea kwa ushirikiano huo kutoka kwa wadau wote, nchi wahisani, makampuni ya dawa, mashirika ya Kimataifa na jamii kwa ujumla.
Amesema kuwa pamoja nchi zinaweza kushinda changamoto zilizopo na kufikia malengo ya Dunia isiyo na magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.