Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, ametoa wito kwa wamiliki na madereva wa pikipiki ya miguu mitatu ( Toyo za umeme)kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi, akisisitiza kuwa ni lazima vyombo hivyo visajiliwe, viwe na bima, na madereva wake wapate leseni halali ili kuendesha shughuli zao kwa uhalali na usalama.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika leo tarehe 21 Mei 2025 katika viwanja vya Mnazi Mmoja, kilichowakutanisha madereva na wamiliki wa vyombo hivyo, Mh. Mpogolo amesema Serikali inalenga kuweka mfumo bora wa usafirishaji wa mizigo na huduma ndogondogo, kwa lengo la kuondoa msongamano, kulinda hadhi ya maeneo ya biashara kama Kariakoo, na kuimarisha taswira ya jiji.
“Tunataka Kariakoo ibaki kuwa soko la kimataifa, lenye mpangilio, usafi, na usalama wa hali ya juu. Hili linawezekana endapo kila mdau atawajibika kwa kufuata sheria. Hatuhitaji kufanya kazi kwa mazoea bali kwa utaratibu unaoleta heshima, ufanisi na maendeleo,” amesema DC Mpogolo kwa msisitizo.
Aidha, DC Mpogolo ametoa muda wa mwezi mmoja kwa wamiliki na madereva wa toyo kuhakikisha wamejisajili, kuwa na bima halali, na kupata leseni ya kuendesha, akibainisha kuwa baada ya kipindi hicho, hatua za kisheria zitaanza kuchukuliwa kwa wale watakaokiuka agizo hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Elihuruma Mabelya, amesema kuwa Jiji linaandaa utaratibu wa kutoa maeneo rasmi ya maegesho kwa ajili ya madereva wa toyo za umeme, ili kurahisisha shughuli zao na kudhibiti hali ya msongamano isiyo rasmi kwenye mitaa ya kibiashara. Alieleza kuwa maeneo hayo yatatolewa kwa utaratibu rasmi na kwa masharti yanayozingatia sheria ndogo za Jiji, ili kuhakikisha madereva hao wanatoa huduma bora bila kuvunja taratibu zilizowekwa.
Hatua hii ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kusimamia mabadiliko katika sekta ya usafirishaji mdogo mjini, hasa katika matumizi ya vyombo vinavyotumia nishati safi kama umeme, ili kuendana na dira ya maendeleo endelevu na jiji la kisasa.