
Mhandisi wa Miundombinu ya Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Leo Magomba, akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mkutano wa 14 wa Jukwaa la usimamizi wa mtandao Barani Afrika unaotarajiwa kufanyika nchini kuanzia Mei 29 hadi 31 2025 Katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa kitaifa wa Jukwaa la Usimamizi wa Mtandao (Internet Governance Forum-IGF Tanzania) Dkt. Naza Kirama akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mkutano wa 14 wa wa Jukwaa la usimamizi wa mtandao barani Afrika unaotarajiwa kufanyika nchini kuanzia Mei 29 hadi 31 2025 Katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mtaalamu wa Usalama wa Mtandao na uchunguzi wa makosa ya Mtandao, Yusuph Kileo akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mkutano wa 14 wa wa Jukwaa la Usimamizi wa Mtandao Barani Afrika unaotarajiwa kufanyika nchini kuanzia Mei 29 hadi 31 2025 Katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
KWA mara ya kwanza Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 14 wa Jukwaa la Usimamizi wa Mtandao (Africa Internet Governance Forum – AfIGF), unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 29 hadi 31 Mei 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo 22 Mei 2025 Mhandisi wa Miundombinu ya Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Leo Magomba,alisema mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu kwa wadau kujadili masuala nyeti yanayohusu maendeleo ya intaneti na teknolojia barani Afrika.
“Mkutano huu ni muhimu sana kwa sababu, kwa mujibu wa takwimu za ITU, ni asilimia 38 pekee ya Afrika wanaotumia intaneti ya uhakika, huku kwa dunia nzima ni asilimia 68. Hii inaonyesha pengo kubwa,” alisema Mhandisi Magomba.
Pia Mratibu wa Kitaifa wa Jukwaa la Usimamizi wa Mtandao (Internet Governance Forum – IGF Tanzania), Dk. Naza Kirama,akieleza zaidi kuhusu mkutano huo mkubwa unaofanyika kwa mara ya kwanza nchini, utanufaisha Tanzania kwa kuwa utahudhuriwa na karibu nchi zote za Afrika pamoja na wawakilishi wachache kutoka ngazi ya kimataifa.
“Tunawapokea wageni kutoka nchi mbalimbali za Afrika tukiwa wenyeji wa Jukwaa la Usimamizi wa Mtandao kwa Kanda ya Afrika. Kutakuwa pia na wawakilishi kutoka nchi tano hadi kumi kutoka nje ya Afrika kwa ajili ya kujadili sera za usimamizi wa mtandao barani Afrika,” amesema Dk. Kirama.
Ameongeza kuwa Tanzania inatarajia kupokea zaidi ya wageni 1,000 kutoka mataifa mbalimbali kwa lengo la kujadili sera na mustakabali wa usimamizi wa mtandao katika bara la Afrika.
“Kama nilivyosema, huu ni mfumo wa kidunia unaoanzia ngazi ya Umoja wa Mataifa, kushuka hadi kanda kama Afrika, kisha kufika katika ngazi za kitaifa. Hapa nchini tuna Jukwaa la Usimamizi wa Mtandao Tanzania (Tanzania Internet Governance Forum – TzIGF), linaloratibiwa kila mwaka,” ameongeza.
Dk. Kirama pia amesema kuwa mkutano huo utahusisha ushiriki wa vijana kupitia jukwaa lao maalum la vijana, pamoja na wabunge ambao nao watakuwa na jukwaa lao kwa ajili ya kujadili masuala ya usimamizi wa mtandao.
“Hapa tutajadili sera za nchi mbalimbali kuhusu usimamizi wa mtandao. Kama mnavyojua, Tanzania inaongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa matumizi ya mifumo ya ulinzi wa kimtandao, na hata kwenye matumizi ya akili bandia (Artificial Intelligence),” amesema.
Kwa upande wake, Yusuph Kileo, Mtaalam wa Usalama wa Mtandao na Uchunguzi wa Makosa ya Mtandao, amesema kuwa mkutano huo umeletwa nchini kutokana na rekodi nzuri ya Tanzania katika usimamizi wa mifumo ya mtandao hususani kwa kipindi cha hivi karibuni.
“Tutajadili mustakabali wa usalama wa mtandao, miundombinu ya kidijitali Afrika, kuongeza ushirikiano baina ya nchi, teknolojia mpya, na namna ya kuhakikisha kila mmoja anapata huduma ya mtandao kwa usawa,” amesema Kileo.