Farida Mangube, Morogoro
Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amesema serikali ya nchi hiyo haina mpango wa kufukua wala kuyarudisha nyumbani mabaki ya miili ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini waliopumzishwa nchini Tanzania, kutokana na heshima na utunzaji mzuri wa maeneo hayo unaofanywa na serikali ya Tanzania.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kuwasili mkoani Morogoro na kutembelea kampasi ya Solomon Mahlangu ( Mazimbu ) Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), eneo ambalo linahifadhi makaburi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini waliokimbilia Tanzania wakati wa vita vya ukoloni.
Mbeki alieleza kuwa Afrika Kusini inatambua na kuthamini mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, hususani msaada wake kwa wapigania uhuru wa nchi hiyo na kwamba makaburi hayo yataendelea kuheshimiwa nchini Tanzania isipokuwa kama ndugu wa marehemu hao wakihitaji kuyarejesha, jambo ambalo litawezekana kwa gharama zao binafsi.
“Tanzania imehifadhi vyema kumbukumbu za mashujaa wetu. Hatuna sababu ya kuyafukua makaburi haya kwa kuwa yako mikononi mwa ndugu wa kweli waliotusaidia wakati wa giza la ukoloni,” alisema Mbeki.
Aidha, Mbeki aliishukuru SUA kwa kazi kubwa ya kuyaifadhi makaburi hayo kwa muda wote, akisema kuwa taasisi hiyo imeonesha uaminifu kwa historia ya Bara la Afrika.
“Tunaishukuru SUA kwa moyo wao wa kizalendo na heshima waliyoonyesha kwa mashujaa wetu. Wamekuwa walinzi wa historia yetu na tunatambua mchango wao mkubwa katika kuihifadhi kwa weledi,” alisema Mbeki.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, alisema serikali ya mkoa itaendelea kulinda maeneo ya kihistoria kama hayo ambayo ni urithi wa harakati za ukombozi wa Afrika.
Hata hivyo alipongeza mpango wa Afrika Kusini wa kutengeneza makala maalumu kwa ajili ya elimu na kumbukumbu ya mashujaa hao, akisisitiza kuwa ni fursa ya kuendeleza fikra za mapambano ya ukombozi wa Afrika kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Tumeona dhamira ya dhati kutoka Afrika Kusini ya kuendeleza fikra za ukombozi na uafrika kupitia vipindi vyao vya kielimu. Huu ni urithi wa pamoja na tutalinda maeneo haya kwa hadhi inayostahili,” alisema Malima.
Akizungumza katika tukio hilo, Makamu wa Rais wa kampuni ya AngloGold Ashanti Afrika, Simon Shayo, alisema ziara hiyo ni sehemu ya mjadala wa 15 wa taasisi hiyo, ambao unalenga kukuza ustawi wa wananchi wa Bara la Afrika kupitia majadiliano ya kihistoria na kimaendeleo.
“Taasisi ya Thabo Mbeki imejikita katika kufufua mwamko wa Afrika katika kufanya maamuzi ya kimkakati kwa mustakabali wa bara letu. Tunaamini kuwa mijadala kama hii inayojumuisha viongozi wa zamani, wataalamu, na vijana ndio njia ya kujenga kizazi kipya chenye matumaini mapya kwa Afrika,” alisema Shayo.
Ziara hiyo ya Rais mstafu wa Afrika Kusini nchini Tanzania ni mashirikiano kati ya taasisi ya Thabo Mbeki Foundation pamoja na kampuni ya AngloGold Ashanti Afrika ambayo imekuwa ikifanya mashirikiano katika kukuza fikra za waafrika katika kujikomboa kifikra.