MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa yanayochochewa na baridi kali na vumbi katika msimu wa Juni hadi Agosti 2025 (JJA).
Magonjwa hayo ni pamoja na ya macho, homa ya mapafu, na yale yanayoathiri mifugo pamoja na upungufu wa maji, malisho kwa mifugo.
Tahadhari hiyo inahusu maeneo ya Magharibi, Nyanda za Juu Kusini-Magharibi, na baadhi ya maeneo ya katika ya nchi.
Akizungumza wakati akitoa utabiri huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema vipindi vya baridi kali vinatarajiwa zaidi mwezi Julai, huku mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida na magharibi mwa Dodoma ikikumbwa na hali ya baridi ya wastani hadi kali huku kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kushuka hadi nyuzi joto 6°C, hasa katika maeneo ya miinuko.
Kwa mujibu wa Dkt. Chang’a msimu wa Kipupwe 2025 utatawaliwa na upepo wa wastani kutoka Kusini Mashariki, na vipindi vya upepo mkali kutoka Kusini vinatarajiwa hasa mwezi Juni na Julai. Upepo huo unaweza kuchochea hali ya vumbi, hali inayoweza kusababisha magonjwa ya macho na athari nyingine za kiafya.
“Licha ya msimu huu kutawaliwa na hali ya ukavu, vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa kujitokeza katika ukanda wa Ziwa Victoria, maeneo ya Pwani, na visiwa vya Unguja na Pemba,” amesema Dkt. Chang’a.
Ameongeza kuwa wakazi wa maeneo hayo wanapaswa kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa kutokana na mabadiliko yasiyotabirika yanayoweza kujitokeza.
Ushauri wa TMA kwa sekta mbalimbali
Kutokana na hali hiyo, TMA inatoa wito kwa wadau mbalimbali kuchukua tahadhari kama ifuatavyo.
Wataalamu wa afya wanatakiwa kuwa tayari kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa magonjwa ya njia ya hewa na mifugo kutokana na baridi kali.Huku wananchi wakishauriwa kuvaa mavazi ya joto hasa asubuhi na usiku, kunywa vinywaji vya moto, na kutumia vifaa kinga dhidi ya vumbi kama miwani na barakoa.
Pia,wakulima wameshauriwa kulima mbogamboga na mazao ya mizizi katika maeneo yanayotarajiwa kupata unyevunyevu au mvua za nje ya msimu.Pamoja na wafugaji kufuata ratiba sahihi za kuogesha mifugo, kuwapatia lishe bora, na kufuata ushauri wa wataalamu wa mifugo ili kudhibiti magonjwa.
Aidha,Sekta ya ujenzi, madini na uchukuzi, zimeelekezwa kutumia fursa ya hali ya ukavu kuendelea na shughuli za maendeleo kwa ufanisi, lakini zizingatie tahadhari dhidi ya upepo mkali unaoweza kuathiri shughuli za baharini na usafirishaji wa majini.
Aidha, TMA imesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta mbalimbali ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza msimu huu, na imetoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na madhara ya baridi kali na vumbi.