Jumla ya Askari 62 waliopandishwa vyeo kwa ngazi ya Koplo, Sajenti, Staff Sajenti na Sajini Meja Mkoani Songwe ambao walihitimua mafunzo ya vyeo hivyo 2024/2025 na kufaulu wamekumbushwa kuwa vyeo hivyo sio zawadi vinaambatana na ongezeko la majukumu katika kazi za kila siku.
Rai hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga wakati wa zoezi la kuwavisha vyeo askari hao kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Camillus Wambura ambalo limefanyika katika Kituo cha Polisi Vwawa Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe Mei 22, 2025.
Katika zoezi hilo Kamanda Senga amewataka askari hao kuvitendea haki vyeo walivyovipata wakati wanatimiza majukumu yao kwa askari na wananchi na kuweka mipaka ya kirafiki na undugu katika kazi ikiwa ni pamoja na kutokuwa na muhali kwa yeyote kwa lengo la kuendelea kutimiza jukumu mama la kulinda raia na mali zao ndani ya Mkoa wa Songwe.
Aidha, amewataka askari hao kuendelea kujiandaa na zoezi la uchaguzi kabla, wakati na baada ya zoezi hilo pia kuhakikisha wanakuwa msitari wa mbele kutoa elimu juu ya umuhimu wa uchaguzi ili ufanyike kwa amani na utulivu kama uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulivyopita.