-Zatoa ajira 200 kwa vijana
-Zachangia ujenzi wa zahanati
📍Ruvuma
Kampuni za uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe katika Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma zimeendelea kusaidia jamii ambapo wananchi wanaoishi jirani na migodi wameendelea kunufaika na ajira huku migodi ikiendelea kuboresha huduma za jamii ikiwa ni pamoja na kuchangia ujenzi wa zahanati hali iliyopunguza adha ya wananchi kufuata huduma za afya katika maeneo ya mbali.
Akizungumza katika mahojiano, Msimamizi wa Kituo cha Mauzo cha Kampuni ya Makaa ya Mawe ya Jitegemee (Jitegemee Holdings Company Limited), Mark Tarimo ameeleza kuwa katika miradi iliyotekelezwa na kampuni hiyo kwa jamii ni pamoja na ujenzi wa vyoo vya shule katika kijiji cha Luagala pamoja na kutoa ajira kwa vijana zaidi ya 200 wanaozunguka maeneo ya mgodini kama mkakati wa kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kupata unafuu wa maisha.
“ Vijana hawa tumeweza kuwapatia ajira katika shughuli za udereva na kufunga maturubai kwenye magari yanayofika kupakia makaa,” amesema Tarimo.
Ameendelea kusema kuwa kampuni ya Jitegemee imeweza kuboresha miundombinu ya mgodi ambapo kwa siku inaweza kuzalisha zaidi ya tani 3000 za makaa, ambayo huchakatwa na kuwauzia wananchi huku wateja wao wakubwa ni kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.
Kwa upande wake Meneja wa kampuni ya Ruvuma Coal Limited, Sanzeh Ntikwa akielezea namna mgodi ulivyoboresha huduma za jamii amesema kuwa mgodi umefanikiwa kujenga madarasa mawili kwenye kijiji cha Paradiso, zahanati na kuboresha ujenzi wa Soko la Paradiso pamoja na kununua vifaa vya michezo kwa vijana.
“Kwenye kijiji cha Sara tumeweza kujenga madarasa mawili, Ofisi ya walimu na zahanati kubwa, kwa sasa tumejipanga kujenga shule ya VETA kwenye kijiji cha Paradiso, ambapo tunasubiri vibali kutoka Serikalini pamoja na michoro ili tuanze ujenzi, vilevile tumenunua basi kwa ajili ya kuwabeba wanafunzi kutoka kijiji cha Paradiso kwenda kwenye shule iliyopo Luagala katika Wilaya ya Mbinga,” amesema Ntikwa.
Naye, Mjiolojia wa kampuni ya Ruvuma Coal Limited, Penina Rububula ambaye ni mmoja wa wananchi walioajiriwa na mgodi huo akielezea manufaa ya ajira yake amesema kupitia ajira yake ameweza kusomesha watoto, kununua kiwanja pamoja na kuendesha maisha yake ya kila siku.
Â